Friday, November 22, 2019

TUSONGE yapiga hatua zaidi kuwafikia wenye ulemavu


Shirika lisilo la kiserikali la TUSONGE, ambalo linajishughulisha na masuala ya Uwezeshaji kiuchumi, Wanawake, Vijana na watu wenye ulemavu mkoani Kilimanjaro, limewafikia watu wenye ulemavu 77 kwa kuunda vikundi vya VICOBA shirikishi kwa watu wenye ulemavu na wasio na ulemavu.

Hayo yalisemwa jana na Mratibu wa mradi wa Vicoba shirikishi Njiapanda Himo, kupitia shirika la TUSONGE Hellena Mushi,  wakati alipokuwa akitoa elimu ya mfumo wa VICOBA  kwa vikundi sita vipya ambavyo vimejiunga na mradi huo.

Bi. Hellena alisema kwa muda mrefu watu wenye ulemavu wamekuwa wakinyanyaswa na kunyimwa haki zao za msingi, hali ambayo ilimefikia hata wakati jamii kuwaficha badala ya kuwapa nafasi ya wao  kuonyesha uwezo wao na kuweza kushiriki katika shughuli  za uzalishaji mali ili waweze kujikwamua kiuchumi na kuondokana na hali ya utegemezi.

Bi. Hellena alisema TUSONGE imeona namna pekee ya kuwasaidia watu wenye ulemavu ili waweze kuondokana na unyanyasaji ni kuwaimarisha kiuchumi kwa kuanzisha miradi ya uzalishaji mali na kuachana na utegemezi.
 “Lengo la kutoa mafunzo haya kwa vikundi hivi vipya  ni kuweza kuwasaidia kuwa na nidhamu ya matumizi ya pesa zao  katika harakati za kujikwamua kiuchumi pamoja na kufahamu namna ya kuviendesha vikundi vyao ili viweze kujiendesha,”alisema Hellena.

 Alisema mafunzo ambayo wameweza kuyatoa ni mfumo wa elimu ya kifedha, usimamizi mzuri wa fedha pamoja na utaratibu wa kujiwekea kumbukumbu halisi za fedha wanazopata, ili vikundi hivyo vitambue umuhimu wa kuweka akiba, sehemu salama za kuweka  akiba na jinsi ya kupanga bajeti na kuweka vipaumbele vya matumizi ya fedha zao.

 “TUSONGE tumeweza kuwafikia watu wenye ulemavu 77 wa moja kwa moja ulemavu  ambao walikuwa wamefichwa majumbani huku watu 182 ni walezi wa watoto wenye na kufanikiwa kuunda vikundi vya VICOBA shirikishi  vya watu wenye ulemavu na wasio na ulemavu  ambapo vikundi 12 vimeundwa  ambavyo vimefanya wanachama kufikia 360.

Alisema mbali na mradi huo kuwakwamua kiuchumi pia unashirikiana na Shirika lisilo la Kiserikali linalotoa huduma za kitabibu na Utengamao kwa watu wenye ulemavu na wale walioko katika hatari ya kupata Ulemavu Tanzania (CCBRT) ambalo limeweza kuwapatia viti mwendo na vifaa saidizi  ili kuweza kushiriki shughuli zote za maendeleo na kuweza kujitegemea.

Kwa upande wake Afisa Mradi Msaidizi Eva Minja alisema shirika hilo limezidi kuweka nguvu katika kuwajengea uwezo kuhusu mikakati ya kuhakikisha kuwa kila mnufaika anaelewa wajibu wake na kuheshimu katiba waliojiwekea Lengo la mradi huu ni kupunguza umasikini na kukandamizwa kwa watu wenye ulemavu pamoja na familia zao kwa kutumia mbinu jumuishi katika jamii ya kata ya njiapanda  Kuboresha na kukuza uwezo wa wanachama wa VICOBA  wakiwemo wanawake, wanaume na wasichana ili kuweza kuzalisha kipato kitakachotumika kukidhi mahitaji yao yatakayoakisiwa .
STORY BY & PHOTO BY: Kija Elias, Moshi
DATE: Novemba 9, 2019


0 Comments:

Post a Comment