Wadau wa Mazingira Manispaa ya
Moshi, mkoani Kilimanjaro wametoa mapendekezo yao kwa Wizara ya Elimu, Sayansi
na Teknolojia nchini, kuhakikisha kwamba wanafunzi watakaoandishwa kuanza
darasa la kwanza mwaka 2020, na wale waliochaguliwa kujiunga na kidato cha
kwanza 2020 kila mwanafunzi aotesha mti wake mmoja ili kuweza
kuboresha hali ya mazingira katika nchi kwa ujumla.
Aidha wadau hao wametoa mapendekezo
yao kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupeleka muswada wa
marekebisho kwa wizara ya Elimu, ambayo itamtaka kila mwanafunzi
atakayejiunga na elimu yake ya msingi na ile ya sekondari kupanda mti wake
mmoja inayotolewa na wadau wa mazingira na kuutunza hadi hapo atakapomaliza
elimu yake ya msingi au ya sekondari.
Hayo yamo kwenye risala iliyosomwa
jana na Sophia John, wakati wa zoezi la uoteshaji miti ya asili katika
maeneo ya taasisi za umma, binafsi na kwenye makazi ya watu, zoezi ambalo
lilifanyika jana katika kata ya Majengo mjini Moshi na kuratibiwa na asasi
isiyo kuwa ya kiserikali inayojishughulisha na utunzaji wa mazingi ya
‘Kibo Environment Conservation Group’ ya Manispaa ya Moshi.
“Tunaiomba serikali kupitia
Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, kutoa tamko ambalo litawaka
walimu wakuu wa shule za msingi na sekondari, kuhakikisha kwamba kila wanafunzi
atakaye andishwa kuanza darasa la kwanza na wale waliochaguliwa kujiunga na
kidato cha kwanza 2020 kila mwanafunzi aotesha mti wake mmoja ili kuweza
kuboresha hali ya mazingira katika nchi yetu, alisema.
Pia wamewaomba walimu wa shule za
msingi na sekondari kuanzisha mashindano ya upandaji wa miti kwa
kila shule za msingi na sekondari ili kila mtoto anayeingia shuleni hapo
anaotesha mti wake mmoja kulingana na idadi ya watoto watakao andikishwa kuingia
darasa la kwanza au sekondari, jambo ambalo litasaidia katika kabiliana
na mabadiliko ya tabia nchi.
Akizindua zoezi hilo la miti ikiwa
ni siku ya kumuenzi aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Mhe; Leonidas
Gama, Afisa Mazingira Manispaa ya Moshi Emanuel John alisema kuwa halmashauri
ya Manispaa hiyo imeanzisha kampeni ya kukamata mifugo yote inayozurura mitaani
na kuharibu miti inayopandwa ili kulinda na kutunza mazingira.
“Wapo baadhi ya wananchi wamekuwa
wakiiachia mifugo yao na kuzurura ovyo, mifugo hiyo imekuwa ikiharibu miti
inayopandwa, serikali imekwisha kutoa maagizo kwa watendaji kata wote
kuhakikisha mifugo itakayoonekana kuzurura inakamatwa na wahusika wanachukuliwa
hatua kali za kisheria,”alisema John.
Alifafanua kuwa serikali imekuwa
ikifanya jitihada kubwa za kupanda miti katika maeneo mbalimbali na
kwa Manispaa ya Moshi zoezi hili lilianzishwa na aliyekuwa mkuu wa Mkoa
Mhe; Leonidas Gama tangu mwaka 2012,”alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kibo
Environment Conservation Group Daniel Mvungi, alisema kutokana na uharibifu
kubwa wa mazingira ikiwemo ukataji miti kwa ajili ya kujipatia nishati ya kuni
na mkuu, asasi hiyo imeanzisha siku maalumu ambayo itakuwa ikifanyika
Novemba 22 ya kila mwaka kupanda miti, ili kumuenzi Mhe; Leonidas Gama,
ambaye alisimama katika kuhakikisha mkoa wa Kilimanjaro unaendelea kuwa
mkoa wa kijani.
“Suala la upandaji miti limepewa
kipaumbele na serikali kuanzia ngazi ya kitaifa hadi ngazi ya chini, na
kwetu sisi Kibo Environment Conservation Group, katika siku ya leo
tumepanda miti zaidi ya 1,000, kwenye shule ya msingi Majengo, taasisi binafsi
na kwenye makazi ya watu, ikiwa ni siku ya kumuenzi aliyekuwa mkuu wa mkoa Mhe;
Leonidas Gama ambaye alikuwa mwanaharakjati katika suala zima la
mazingira,’alisema Mvungi.
Naye Kamishna wa Skauti
Tanzania Manispaa ya Moshi Mbena Emerensiana, alisema upandaji wa miti ni
njia moja wapo ya utunzaji wa mazingira na kulinda uoto wa asili hivyo Skauti
Tanzania itaendelea kuwa mstari wa mbele katika kushiriki kupanda miti ambayo
itasaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
STORY & PHOTO BY: Kija Elias, Moshi
DATE: Novemba 23, 2019
0 Comments:
Post a Comment