Katika miongo kadhaa iliyopita,
uvaaji wa wigi umekuwa fasheni katika sekta ya urembo na hutumika hususan na
wanawake. Ingawa uvaaji wa wigi huwafanya wanawake hao kuonekana mithili ya mtu
aliyevaa kofia ngumu (helmet), lakini yaonekana ni mapendeleo ya wengi.
Wanaume wengi hujiuliza ,
"Ni kwanini kinamama hupendelea kuvaa wigi na kusuka nywele za bandia?,
wakati hupendeza na kuwa warembo zaidi wakiwa na nywele zao za asili"
Wigi huvaliwa zaidi na kinamama
wenye asili ya Afrika au Wamarekani wa asili ya Afrika. Lakini tukiangalia moja
ya chimbuko hasa la uvaaji wigi ni ubaguzi uliokuwepo wakati wa utumwa ambapo
wale wenye ngozi nyeupe na nywele shombeshombe walipewa kazi za ndani na wale
wasio na ngozi nyeupe na nywele zisizo shombeshombe walifanyishwa kazi ngumu za
mashambani. Watumwa waliopelekwa barani Amerika hawakuweza kuzihudumia nywele
zao kutokana na hali ngumu, na mabwenyenye waliwashusha hadhi na kuwavunja moyo
kwa kuwaambia hawakuwa na nywele bali ni "manyoya".
Lakini sababu nyingine
inayodhaniwa kuwaathiri wanawake wa asili ya Afrika ni fikra kuwa mwanamke
mwenye nywele ndefu pengine hadi mgongoni ni mrembo zaidi. Pia siku hizi
warembo na wanaoshiriki katika mashindano ya urembo hujaribu kurefusha nywele
zao ili kuwa na viwango na aina za mitindo ya ughaibuni.
Pamoja na kuwa wanawake
wanajaribu kuwa warembo kwa uvaaji wa wigi, zifuatazo ni baadhi ya hasara au
madhara kiafya ya uvaaji wigi na usukaji wa nywele za bandia.
Uvaaji wa wigi au nywele za
bandia waweza kukusababishia mzio(allergy), endapo malighafi au kemikali
zilizotumika kutengeneza wigi hiyo zitasisimua mfumo wa kinga ya mwili wa
mvaaji.
Kupata mba ni tatizo jingine
kutokana na uvaaji wigi, hii hutokana na kukosekana kwa hewa ya kutosha ya
Oksijeni katika ngozi ya kichwa(scalp hypoxia) na katika tishu za shina la
nywele. Kwa hiyo kama utaamua kuvaa wigi uhakikishe imetengenezwa kwa viwango
vya ubora unaotakiwa na inapitisha hewa ya kutosha ya Oksijeni.
Pia waweza kunyonyoka nywele
hata kama una nywele nzuri zenye afya, na kama utachagua kuvaa wigi na unataka
kuepuka madhara hakikisha kuwa nywele zako ni safi, usilazimishe kuvaa wigi
iliyo ndogo na yenye kubana sana, hakikisha unapata muda wa kupata hewa na
nywele zako zinapakwa mafuta kuepuka ukavu wa ngozi ya kichwa na nywele
kukatika.
Maumivu ya kichwa ni tatizo
ambalo laweza kusababishwa na uvaaji wigi au usukaji wa nywele bandia. Wigi
iliyo ndogo husababisha mkandamizo kichwani na kusababisha maumivu ya kichwa ya
mara kwa mara.
Upotevu wa muda na fedha ni
dhahiri kwa kuwa ufumaji wa nywele za bandia waweza kuchukua muda mrefu,
itamlazimu mvaaji wigi kubadili kwa kununua mpya kila baada ya muda fulani au
kuwa na wigi nyingi kwa ajili kubadili kulingana na fasheni.
Harufu mbaya huweza kujitokeza
endapo mba na jasho vitachanganyikana na hupelekea uwepo wa bakteria au fangasi
na kusababisha muwasho mkali, hii yaweza kumkosesha raha mvaaji wigi na mwenye
kufuma nywele za bandia hasa pale anapokuwa katika majumuiko ya kijamii.Kama
utachagua kuvaa wigi hakikisha nywele zako zinasafishwa na shampoo au sabuni,
zinakaushwa vizuri na kupakwa mafuta.
Endapo mwanamama atachagua
kuvaa wigi,asisahau kuwa nywele zake za asili zinahitaji matunzo,na azingatie
wakati wa kununua wigi au nywele za bandia, ahakikishe ananunua yenye ubora
unaotakiwa ili kuepuka madhara ya kiafya anayoweza pata kutokana na uvaaji wigi
au anapofuma nywele za bandia.
CREDIT
TO: Dr.Joh Positive Health and Wellness
0 Comments:
Post a Comment