Thursday, November 21, 2019

Morocco ni taifa la namna gani?

Morocco ni taifa lenye mamlaka halali ya kisheria ambalo lipo katika ukanda wa Maghreb, katika Afrika ya Kaskazini. 
Limepakana na bahari ya Mediterrania kwa upande wa kaskazini na bahari ya Atalantiki kwa upande wa Magharibi. 
Pia linapakana na Algeria kwa upande wa kaskazini Mashariki na Mashariki, Mauritania kwa upande wa Kusini Mashariki. Aidha Taifa hili linaendelea kushikilia maeneo ya Ceuta, Melilla na Peñón de Vélez de la Gomera ambayo yanazungumza lugha ya Kihispaniola. 
Mji Mkuu wa Morocco ni Rabat na mji wa pili kwa ukubwa ni Casablanca. Lina miji mingine kama Marrakech na Agadar. Lina ukubwa wa kilometa za mraba 710,850 huku wakazi wake wakifikia milioni 35.5. 
Historia ya taifa hilo inarudi mbali sana hadi mwaka 788 B.K wakati wa utawala wa Mfalme Idris I ambaye ndiye aliyeweka mipaka  ya kwanza kabisa ya eneo hilo kuwa dola huru. 
Kwa sasa Morocco bado inaendelea kushikilia eneo la Sahara ya Magharibi ambalo linataka kujitenga. 
Eneo hilo awali lilikuwa likikaliwa na Wahispaniola. Baada ya makubaliano ya kujiondoa katika kushikilia hatamu za kuwa mikononi mwake Morocco na Mauritania ziliingia vitani mwaka 1975 kwa alijili ya eneo hilo kila moja ikilitaka kwa udi na uvumba. 
Mauritania ilijiondoa katika mgogoro huo mwaka 1979 na vita ilisimama kabisa mwaka 1991. Morocco hadi sasa bado inashikilia eneo la theluthui mbili huku juhudi za kimataifa zikiendelea kwa ajili ya kuishawishi Morocco kuachana na songombingo hilo la kuikalia Sahara Magharibi. 
Utamaduni wa Morocco ni mchanganyiko wa  jamii ya Waberiberi, Waarabu na Wayahudi wa Serphardi, Afrika Magharibi na baadhi ya mataifa ya Ulaya. Ilijipatia uhuru wake Aprili 7, 1956.
Imetayarishwa na Jabir Johnson.........................Novemba 21, 2019

0 Comments:

Post a Comment