UHARIBIFU wa mazingira
ni suala linalopigwa vita na wadau wote wa mazingira wakiwemo wale wa ndani na
nje ya nchi kwani licha ya kuharibu mazingira pia husababisha maafa ikiwemo
mabadiliko ya hali ya hewa na uharibifu wa miundombinu.
Yako mazingira
mbalimbali yanayosababisha uharibifu wa mazingira kama vile kutotunzwa vizuri
kwa mazingira hususani yale ya asili, jambo ambalo limekuwa
likisababisha kutokea kwa mafuriko na mabadiliko ya hali ya hewa.
Katika kuhamasisha
utunzaji wa mazingira, asasi isiyo kuwa ya kiserikali inayojishughulisha na
utunzaji wa mazingi ya ‘Kibo Environment Conservation Group’ ya Manispaa
ya Moshi mkoani Kilimanjaro inatarajia kuzindua kampeni ya upandaji miche
ya miti Novemba 22 mwaka huu, kwa lengo la kumuenzi aliyekuwa Mkuu wa
Mkoa wa Kilimanjaro Leonidas Gama, ambaye ndiye alikuwa mwanaharakati
mkubwa kuhakikisha mkoa huo unaedelea kuwa mkoa wa kijani.
Akizungumza jana
vyombo vya habari mjini Moshi, Mkurugenzi wa asasi hiyo Daniel Mvungi alisema,
kutokana na uharibifu kubwa wa mazingira, asasi hiyo imeanzisha siku
maalumu ambayo itakuwa ikifanyika Novemba 22 ya kila mwaka, ili kumuenzi Leonidas Gama, ambaye alisimama kidete kuhakikisha mkoa wa Kilimanjaro
unaendelea kuwa mkoa wa kijani kwa kupanda miti kwa wingi.
Leonidas Gama enzi za uhai wake |
Alisema katika siku
hiyo miti zaidi ya 1,000 itapandwa katika maeneo mbalimbali ya taasisi za umma
na binafsi, ambapo alisema wao kama wadau wa mazingira wanapata wakati
mugumu hasa wanapoona kuwa mazingira yanaendelea kuharibiwa kwa kukatwa hovyo
na kukosekana kwa miti ambayo huvuta mvua.
Katika hatua nyingine
Mvungi alisema miti hiyo itapandwa katika shule ya msingi majengo, ofisi
ya mtendaji kata, na kwenye makazi ya watu, na miti mingine itagawiwa kwa
wananchi wa maeneo hayo ili waweze kupanda katika makazi yao.
“Kibo Sports Club
tumekuwa tukijihusisha na zoezi la utunzaji wa mazingira tangu mwaka 2010
kupitia kitengo chetu cha Kibo Environment Conservation Group, ambapo tangu
tuanze na zoezi hili la upandaji miti zaidi ya miti 10,000 tumekwisha kuipanda
katika maeneo mbalimbali,”alisema Mvungi.
Alisema Kibo
Environment Conservation Group, imeanza kulipa uzito unaostahili suala la
uharibifu wa mazingira ambao umelikumba taifa kwa kiasi kikubwa katika miaka ya
hivi karibuni, huku akitoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika
uzinduzi wa kampeni hiyo itakayozinduliwa na afisa mazingira Mkoa wa
Kilimanjaro shughuli ambayo itakayofanyika katika ofisi za ofisi ya mtendaji wa
Kata ya Majengo.
STORY BY & PHOTO BY: Kija Elias, Moshi
DATE: Novemba 20, 2019
0 Comments:
Post a Comment