Tuesday, November 19, 2019

Prof. Mbarawa azichimba mkwara Bodi za Mamlaka za Maji


Waziri wa Maji, Prof. Makame Mbarawa, amesema hatasita kuzifuta bodi za Mamlaka za maji nchini ambazo  zitaonyesha  kushindwa kusimamia ukusanyaji wa mapato na badala yake bodi hizo kuwa sehemu ya kulipana posho za vikao,  safari na sherehe.

Waziri Mbarawa aliyasema hayo Novemba 16 mwaka huu mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, wakati alipokuwa akizindua bodi mpya ya Mamlaka ya majisafi na Usafi wa Mazingira mjini Moshi MUWSA.

Alisema bodi za Mamlaka za maji nchini hazijaweza kufanya kazi yake inayostahili  ya usimamizi wa ukusanyaji wa mapato na badala yake zimekuwa  ni bodi za kulipana posho za vikao, kufanya sherehe za kupongezana na safari.
“Bodi ni chombo muhimu  kwenye taasisi yeyote , bodi kama itatekeleza vizuri, itasimamia vizuri, itaonyesha vema katika kuzisimamia Mamlaka hizi taasisi husika zinaweza kufanya vizuri zaidi,” alisema.

Aliongeza kusema kuwa  na  “Mimi nataka kuwa mkweli bodi za Mamlaka za maji kote nchini hazijafanya  kazi zake inayostahili, mtazamo wangu , kwa badi ambazo zitashindwa kusimamia makusanyo ya mapato nitazifuta.

Waziri Prof Mbarawa  alisema endapo bodi zitasimamia vizuri zinaweza kujenga miradi mingi  ya maji na kuondoa kero kwa watanzania, zitaweza kuondoa malalamiko  baina ya wafanya kazi kwani wataweza kuwalipa  fedha zao kwa wakati.

“Mmekabidhi Mamlaka hizi  ni lazima , msizitumie kwa ajili ya kulipana posho, sherehe na safari,  kwa hili nitakuwa mkali kweli , hatuwezi kuhangaika na mradi wa Sh milioni 700 halafu Mamalaka inakuja Wizarani  kuomba fedha nitawafukuza.”alisema.

Alifafanua kuwa  wakati  anaingia kwenye Wizara  ya Maji  alianza kuzifuatlia Mamlaka  Saba , ikiwemo DAWASCO, AUWSA, Mamlaka ya mji mdogo Kilwa, MUWSA, MORUWASA, Mbeya ambapo kwa Dawasco pekee ilikuwa ikikusanya Sh bilioni 8.4

“Niliwaambia haiwezekani Dawsco mkawa na miradi mingi halafu makusanyo yanakuwa bilioni 8.4 waliweza kuongeza na sasa wanakusanya Sh bilioniu 10 hadi 11,"alisema.

Alisema Muwsa aliwaagiza kukusanya Sh milioni 900 lakini hadi sasa wameshindwa kufikia lengo hili licha ya kuwepo kwa miradi mingi ya maji,  hivyo kuziagiza bodi  na watendaji  wake kubadilika na kuondokana na kufanya kazi za kimazoea.

“Nataka kuwaeleza ukweli kabisa mimi sitaki kuwa Waziri wa kulipa madeni, nataka niache historia ya kuwa Waziri ambaye anaacha alama, haiwezekani mradi unaharibika unahitaji kununuliwa nati halafu Watu wanakuja Wizarani kuomba fedha jambo hili kwangu sitaki kabisa kulisuikia,”alisema.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Prof. Kitila Mkumbo, alisema  katika  kubana matumizi Serikali kupitia Wizara yake  imezifuta Mamlaka za Maji safi na Usafi wa Mazingira 76 na maeneo yake yatahudumiwa na Mamlaka za makao makuu ya mikoa 25, zilizoundwa na kuongezewa majukumu ya utoaji huduma.

“Tulikuwa Mamlaka  za maji hapa nchini zipatazo 159  ambazo nyingi zilikuwa ni utitiri, zilikuwa ziongeza gharama za uendeshaji tumeamua kuzifuta na kubakiwa na Mamlaka 83 lengo ni kuwa na Mamlaka ndogo ambazo zitaweza kufanya kazi kwa ufanisi,”alisema Prof Mkumbo.

Awali akizungumza Mwenyekiti wa bodi ya MUWSA aliyemaliza muda wake Prof. Faustine Bee alisema   wakati anaingia  kwenye Mamlaka hiyo aliikuta ilikuwa na uwezo wa kuzalishaji maji kwa siku lita za ujazo 35,000  ambapo kwa sasa uwezo wa uzalishaji maji uliongezeka na  kufikia  lita za ujazo 52,000.

STORY BY: Kija Elias, Moshi
DATE : Novemba 16, 2019

0 Comments:

Post a Comment