Novemba 20, 1942 alizaliwa
mwanasiasa wa Marekani ambaye alihudumu kama makamu wa rais wa 47 wa taifa hilo
kutoka mwaka 2009 hadi 2017.
Huyo ni Joe Biden. Jina lake halisi ni Joseph
Robinette Biden Jr. Biden aliwahi kuliwakilisha jimbo la Delaware katika nafasi
ya Useneta kutoka mwaka 1973 hadi 2009 kwa tiketi ya chama cha Demokratiki.
Biden ameshatangazwa na chama chake kuwa katika uchaguzi mkuu wa 2020 nchini
humo atakuwa mgombea wa urais kupambana na Donald Trump wa Republican.
Biden hakupata
mafanikio alipowania kuteuliwa kugombea nafasi hiyo mwaka 1988 na 2008. Biden
alizaliwa katika Hospitali ya St. Mary’s huko Scranton, Pennsylvania kutoka kwa
wazazi Catherine Eugenia Biden na Joseph Robinette Biden Sr.
Alikuwa mtoto wa
kwanza kati ya wanne kutoka katika familia hiyo ya kikatoliki akiwa na dada na
kaka zake wawili.
Mama yake ni kutoka katika uzao wa Ireland. Baba yake alikuwa
ni mtu mwenye uwezo kabla ya kuzaliwa kwa Biden. Wakati wa ujio wake Biden
duniani alijikuta katika wakati mgumu kiuchumi
huko Scranton.
Mwanzoni mwa miaka 1950 baba yake aliamua kuondoka huko
na kwenda Claymont, Delaware ambako aliishi kwa miaka kadhaa kabla ya kuhamia
maeneo Wilmington, Delaware.
Baba yake alikuwa muuzaji wa magari yaliyotumika
na Joe Biden Sr alifanikiwa sana katika biashara hiyo na kuifanya familia yake
kuwa na maisha ya kati.
Alipokuwa mwanafunzi Agosti 27, 1966 alimwoa Neilia
Hunter ambaye alimzalia watoto watatu, mkewe huyo alifariki dunia mwaka 1972
akiishi naye kwa miaka mitano tu.
Mnamo mwaka 1977 alimwoa Jill Jacobs aliye
naye mpaka sasa na Biden alikuja kuwa
mwanasheria mwaka 1969 na alichaguliwa na Baraza la Kaunti ya NewCastle mnamo
mwaka 1970 kuwa mwanasheria.
Alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa seneta wa
Marekani mnamo mwaka 1972 na kuweka rekodi ya kuwa seneta wa sita kushika
nafasi hiyo katika umri mdogo kwenye historia ya taiafa hilo.
Biden
amechaguliwa mara sita kuongoza Delaware hadi alipokuja kuachia nafasi hiyo ili
aweze kuwania umakamu wa Rais 2009. Biden anashika nafasi ya nne ya maseneta
wakongwe nchini Marekani.
Biden alikuwa mpinzani mkuu wa vita ya Ghuba ya mwaka
1991 lakini ndiye aliyeishauri Marekani na NATO kuingilia kati vita ya Bosnia
mwaka 1994 na 1995.
Pia alipiga kura ya
kuidhinisha vita dhidi ya Iraki mnamo mwaka 2002 lakini alipinga kuongeza zaidi
wanajeshi wa Marekani katika miji ya Baghdad na Al Anbar mwaka 2007 wakati wa
utawala wa George W. Bush.
Mnamo mwaka 2008 Biden alikuwa mgombea mwenza wa
Barack Obama aliyekuwa akiwania urais wa taifa hilo.
Baada ya uchaguzi huo
Biden aliweka rekodi ya kuwa makamu wa rais wa kwanza mkatoliki kushika nafasi
hiyo katika historia ya Marekani.
Akiwa katika nafasi hiyo alishuhudia
mabadiliko makubwa katika miundombinu ya taifa hilo huku akichangia pakubwa
sera za nje za Marekani ambapo walifanikiwa kuyaondoa majeshi ya Marekani
nchini Iraki mnamo mwaka 2011.
Uwezo wake wa kukaa chini na wapinzani wao
Republicans ulisaidia sana utawala wa Obama kupitisha baadhi ya sheria zenye
manufaa kwa taifa hilo. Yeye na Obama walichaguliwa tena mwaka 2012 kuongoza
taifa hilo. Oktoba 2015 Biden alitangaza kwamba hatawania nafasi ya Urais
katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2016.
Januari 2017 Obama alimtunuku Biden medali
ya Uhuru inayotolewa na Rais wa Marekani kwa yeyote alionyesha upekee. Baada ya
kumaliza kipindi cha pili cha kuwania nafasi hiyo Biden alienda zake katika Chuo
Kikuu cha Pennsylvania kuungana na wakufunzi wengine katika mojawapo ya kitivo
chuoni hapo.
Aprili 25, 2019 alitangaza kwamba atawania Urais katika uchaguzi
mkuu wa mwaka 2020.
0 Comments:
Post a Comment