Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Dkt. Anna Mghwira akiwa katika picha ya pamoja na watu wenye mahitaji maalumu pamoja na wadau wa mawasiliano Tanzania TCRA. |
Tanzania kama zilivyo nchi nyingine
za Kiafrika watu wenye ulemavu (WWU) ni miongoni mwa watu wanaobaguliwa
na kuishi katika mazingira magumu katika jamii zao.
Katika kuliona hilo, Mamlaka ya
Mawasiliano nchini TCRA Kanda ya Kaskazini iliamua kusaidia juhudi za kupigania
na kutetea haki za watu wenye ulemavu zilizomo katika mkataba wa Umoja wa
Mataifa Kuhusu Haki za Watu wenye Ulemavu na Sheria ya Mwaka 2010 kuhusu Watu
wenye Ulemavu Tanzania.
Msukumo wa TCRA upo katika kufanya
ushawishi na utetezi ili serikali na wadau mbalimbali watekeleze mkataba
na sheria ambayo ina lengo la kuleta mabadiliko chanya ya kimuundo na ufanyaji
maamuzi ili kujumisha haki za Watu wenye ulemavu.
Mamlaka ya Mawasiliano nchini TCRA
Kanda ya Kaskazini imefanya mkutano wake wa siku moja na watu wenye
mahitaji maalum Manispaa ya Moshi, kwa lengo la kutoa elimu kuhusu utumiaji wa
huduma za mawasiliano na namna ya kukabiliana na changamoto katika kutumia
huduma za mawasiliano.
Mhandisi Mwandamizi kutoka TCRA
Kanda ya Kaskazini Jan Kaaya, anasema kundi la watu wenye ulemavu lina nafasi
yake katika jamii, lina haki kama ilivyo kwa makundi mengine ya kupata habari
kupitia njia yoyote ya mawasiliano hivyo ni wajibu wa TCRA kutoa elimu kama
hiyo ili kuelewa namna watakavyoshiriki kupata habari kwa njia ya mitandao
“Mafunzo hayo ni kwa ajili ya
kuwapatiwa elimu ya kukabiliana na changamoto wanazokutana nazo katika
kutumia bidhaa za mawasiliano, kwani watu hawa wamekuwa wahanga wakubwa katika
kutumia mawasiliano kutokana na ulemavu walionao,”amesema Mhandisi Kaaya.
Mhandisi Kaaya amesema kundi hilo
kama wadau wao muhimu wamekuwa na changamoto nyingi katika kutumia bidhaa
za wasiliano, kwani baadhi yao hawana uelewa katika suala la changamoto za
mawasiliano, hali inayopelekea kuathirika na vitendo vya wizi wa mitandaoni.
Amesema TCRA itaendelea kutoa
huduma bora kwa wadau wao , wateja na jamii kwa ujumla ili kuhakikisha wanapata
uelewa wa kujikinga na vitendo vya wizi wa mitandao, kwani matukio mengi
ya wizi wa mitandao yamekuwa yakiripotiwa na wateja wao wakiwamo watu wenye
mahitaji maalumu hivyo wameamua kulielimisha kundi hilo kuhusu kujikinga na
vitendo hivyo.
Mwezeshaji wa warsha
hiyo ambaye pia ni Afisa Masoko kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Kanda ya
Kaskazini Lucy Mbogoro, amesema Warsha hiyo imelenga kutoa elimu inayohusiana
na huduma za mawasiliano, kutokana na kubainika kuwepo kwa matumizi mabaya ya
mawasiliano ya simu.
“Katika mkutano huu tumetoa
tahadhari ya changamoto zilizopo katika mawasiliano ambazo watu wenye mahitaji
maalumu wamekuwa wakikutana nazo hasa katika kutapeliwa, njia mojawapo ya
kupunguza tatizo hili ni kumsaidia mtumiaji, mfano kapokea ujumbe wa kutakiwa
kutuma fedha kwa namba asiyoifahamu asitekeleze kwanza na nini anatakiwa
kufanya kabla ya kutekeleza jambo hilo” amesema Mbogoro.
Mhandisi Mwandamizi kutoka TCRA Kanda ya Kaskazini Jan Kaaya. |
Anafafanua kuwa “Baadhi ya mtu
mwenye mahitaji maaalumu anaweza kuwa amejiunga kifurushi na kabla
hajakitumia akakata, na yeye bila kuelewa kuwa anahaki ya kujua, lakini ana
amua kununua vocha nyingine na kujiunga tena bila yeye kujua, tumewaelekeza
kuwa wanapokutana na changamoto kama hiyo, kwanza anatakiwa kuhoji na
tumewaelekeza mamlaka ilipo kwa ajili ya kuja kupata msaada zaidi pindi
anapokuwa hajaridhika na majibu ya mtoa huduma” amesema Mbogoro.
Akifungua warsha ya siku moja
iliyoandaliwa na Wadau wa Mawasiliano TCRA Kanda ya Kaskazini na kuwashirikisha
Watu wenye mahitaji Maalumu, Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Dkt Anna Mghwira
amesema matumizi ya simu yasiwe mzigo kwa wananchi haswa kwenye eneo la
mihamala ya fedha.
Dkt. Mghwira amesema serikali
inafahamu fika kwamba makampuni ya simu yatahitaji fedha kwa ajili ya
uendeshaji lakini makapuni hayo yasitumike kuwaumiza wananchi bali yawe na
gharama nafuu kwa watumiaji.
Wanafunzi wa Chuo cha Ufundi Moshi, wakiwa katika warsha ya mafunzo inayotolewa na TCRA. |
Katika hotuba yake Dkt. Mghwira
ameyataka makampuni yote ya simu kuangalia uwezekano wa kupeleka mawasiliano
vijijini kwani maeneo mengi ya wananchi waishio vijijini wamekuwa wakiteseka
kutoka kata moja kwenda kata nyingine kufuata huduma ya mawasiliano.
“Asilimia kubwa ya mazao yanayoletwa
mjini kutoka vijijini, yanahitaji sana kuwa na huduma ya mawasiliano
yenye uhakika , lakini cha kushangaza ukienda maeneo ya vijijini bado kuna
maeneo ambayo hayana mawasiliano kabisa,”anasema Dkt. Mghwira.
Hata hivyo Dkt. Anna Mghwira
ameitaka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kujitanua zaidi hadi katika
maeneo ya vijijini ili na wao waweze kupata elimu kama hiyo, kwani maeneo
hayo bado kuna changamoto ya upatikanaji wa mitandao hususan katika maeneo ya
vijijini na kuwaomba TCRA kutembelea katika maeneo ya vijijini ambako
kuna changamoto kubwa ya mawasiliano.
Naye Krypton Mmanga ambaye ni
mlemavu wa macho, alisema watu wengi wenye ulemavu wamekuwa wakifanyiwa vitendo
vya wizi wa kimtandao, hali ambayo imekuwa ikizidisha kwao maisha kuwa magumu
zaidi.
“Unapokwenda kwenye kampuni ya simu
kwa ajili ya kutoa fedha ambayo nimetumiwa na mzazi wangu ukifika
wanakuomba namba ya siri ya simu yako, unawatajia, wakishafungua
wanajihamishia kwanza ile hela kwenye simu yao, halafu wanakwambia hii
hela yako salio lake halifai kutoa kiasi ulichokitaja?... wakati mimi mzazi
wangu ameniambia kanitumia kiasi flani jambo hili linatuumiza
sana,”alisema.
Aidha Mmanga
amependekeza kwa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), kuwa na
dawati maalumu la kuwahudumia watu wenye mahitaji maalumu pamoja na
kuwepo kwa wataalamu wa alama jambo ambalo litasaidia watu walemavu
kupata huduma kwa urahisi.
Alifafanua kuwa Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA),
wanapaswa kufanya kazi kwa ukaribu zaidi ili kuwafikia watu wenye mahitaji
maalumu ya mtu mmoja mmoja kulingana na ulenavu walionao.
“Kuna kauli ambazo zimekuwa
zikitolewa na baadhi ya wafanyakazi wa NIDA wamekuwa wakitutolea sisi watu
wenye ulemavu majibu yenye kutuudhi, sisi ni watu wenye ulemavu,
pindi tunapofuiatilia vitambulisho vyetu… tumekuwa tukijibiwa kwa lugha
chafu jambo hii kwa kweli siyo sahihi,”alisema Mmanga kwa masikitiko makubwa.
Ahadiel Sowene Mphuru ni mlemavu wa
kutokusikia kutoka shule ya ufundi Moshi, anaiomba TCRA kuzidi kutoa elimu kwa
watu wenye mahitaji maalumu hali ambayo itasaidia katika kutatua changamoto
mbalimbali ambazo zimekuwa zikiwakabili katika maeneo yao.
Pia aliiomba TCRA kufuatilia kwa
karibu malalamiko ambayo yamekuwa yakitolewa katika ofisi zao na kuhakikisha
wahusika wa wizi wa mitandao wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria
ili kudhibiti tatizo la wizi wa mitandao kwa watu wenye ulemavu.
“Niwashukuru sana TCRA kwa sababu
hapo mwanzo sikuwa na uelewa na kuna vitu nilikuwa na fanyiwa na mitandao ya
simu lakini sikujua kama sitendewi haki lakini kwa sasa nimeelewa vizuri, na
ukizingatia sisi watu wasioona ndio waathirika katika vitendo vya wizi
mitandaoni” amesema Mphuru.
Afisa Masoko kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Kanda ya Kaskazini Lucy Mbogoro |
Mwenyekiti wa Chama Cha Wasioona
Manispaa ya Moshi (TLB), Ezron Macha ameiomba serikali kuwepo na dawati maalumu
litakalowawezesha watu wenye ulemavu kufika kwa urahisi na kuhudumiwa kwa
wakati.
Macha ambaye pia ni mlemavu wa macho
amesema makundi maalumu yanachukua asilimia 10 ya watu wote nchini na kwamba
kumekuwepo na utapeli kwenye mitandao ya simu hivyo ni vyema TCRA
ikawadhiti watu ambao wamekuwa wakitumia mitandao ya simu kwa ajili ya
kuwatapeli watu hususan wasoona kwani huamini kuwa wanachokitumia huwa ni kweli
na hivyo kujikuta wakituma fedha pasipo kujua.
Katibu wa Chama Cha Wasiosikia mkoa
wa Kilimanjaro Christina Shirima, ameishukuru TCRA kwa kuwapatia elimu hiyo,
pia amesema changamoto kubwa waliyonayo ni kushindwa kupata vitambulisho vya
NIDA kwa hivyo kukwamisha zoezi la kusajili laini zao za simu kwa wakati.
Katika Mkutano huo uliofanyika
katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro
uliwashirikisha watu wenye mahitaji maalumu kutoka Manispaa ya Moshi zaidi ya
150, wakiwemo watu wenye ulemavu wa macho, albino na viziwi.
Imetayarishwa
na Kija Elias...................Novemba 25, 2019
0 Comments:
Post a Comment