Novemba 25, 1881 alizaliwa
Papa Yohane wa 23 (Pope John XXIII). Alishika madaraka hayo ya juu katika
Kanisa la Katoliki kuanzia Oktoba 28, 1958 hadi kufariki kwake Juni 3, 1963.
Jina
lake halisi ni Angelo Giuseppe Roncalli. Papa Yohane wa 23 alishika madaraka
hayo kuliongoza kanisa hilo lenye makao yake makuu jijini Vatican. Angelo Giuseppe alikuwa ni mojawapo wa watoto
13 wa familia moja ya kilimo iliyokuwa ikiishi kijijini huko Lombardy nchini
Italia. Aliiingia katika huduma kwenye kanisa hilo Agosti 10, 1904. Akiwa
katika kanisa hilo ametumikia katika nafasi mbalimbali katika maeneo tofauti
ikiwamo Bulgari, Ugiriki na Uturuki. Januari 12, 1953 Papa Pius wa XII alimtawaza Roncalli kuwa
Kardinali wa Santa Prisca huko huko nchini Italia. Roncalli hakutarajiwa
kuchaguliwa kuwa papa. Aliingia katika nafasi hiyo akiwa umri wa miaka 76 kwa
kura 11. Baada ya kuchaguliwa kwake alionyesha usawa miongoni mwa binadamu
aliposema, “ Sisi sote tumeumbwa kwa mfano wa sura ya Mungu na hivyo basi sote tunafanana
na Mungu.” Papa Yohane XXIII alijitahidi kushirikiana na makanisa mengine. Pia
alipambana kuhakikisha kuwa maaskofu wa kanisa hilo nchini Italia hawajiingizi
katika siasa. Aliondoa utaratibu wa enzi wa kuwa na makadinali 75 na kuwateua
kufikia 85. Alitumia nafasi hiyo kuwatawaza makadinali kutoka Afrika, Japan na
Ufilipino. Alitangazwa kuwa Mtumishi wa Mungu na Papa Paulo VI aliyechukua
mikoba ya kuliongoza kanisa hilo baada ya kifo chake Novemba 18, 1965. Kwa mchango
wake katika kanisa katoliki Julai 5, 2013 Papa Francis anayeliongoza kanisa
hilo kwa sasa alimtangaza Papa Yohane XXIII kuwa Mtakatifu. Kwa sasa Papa
Yohane XXIII anafahamika kama Papa Mzuri kwa kiitaliano “il Papa buono.”
0 Comments:
Post a Comment