Watu 10 wamepoteza maisha
papo hapo na wengine kujeruhiwa katika
ajali ya basi iliyotokea katika barabara ya Harare-Bulawayo nchini Zimbabwe.
Ajali hiyo imetokea katika
eneo moja lililopo Kwekwe na Gweru nchini humo ikihusisha mabasi mawili yaliyogongana
uso kwa uso.
Waziri wa Nchi katika eneo
la Midlands anayehusika na Mambo ya Ndani ya Majimbo Cde Larry Mavima
amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo.
Mavima amesema ajali hiyo
imetokea majira ya saa 10:30 alfajiri wakati basi la kampuni ya Mandeep Tours ikitokea
Afrika Kusini kwenda Gokwe ilipogongana uso kwa uso na Kampuni ya mabasi ya Govasberg
iliyokuwa ikienda Gweru.
Aidha waziri huyo amesema
wakati wakikaribia kibao cha kilometa 232 dereva wa Mandeep alipoteza mwelekeo
wa basi lake baada ya taa zilizokuwa kali za basi la Govasberg hatua
iliyosababisha mabasi hayo kugongana.
Taarifa kutoka nchini humo
zinasema hadi sasa maofisa wa polisi wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo
lililotokea jana alfajiri.
Mavima amesema miili ya
marehemu imepelekwa katika hospitali ya Kwekwe.
Hata hivyo Waziri wa
Serikali za Mitaa, Kazi za Jamii na Nyumba Cde July Moyo amesema ajali hiyo ni
maafa ya kitaifa na kwamba familia zilizokutwa na zahama hilo zitapewa usaidizi
kutoka serikali.
Aidha ametoa wito kwa
madereva kuthamini maisha ya watu pindi wanapoendesha vyombo vya moto na
kuzingatia sheria za usalama barabarani kwani ajali iliyotokea ilikuwa na
uwezekano wa kuthibitiwa kabla ya maafa hayajatokea.
Msemaji wa Polisi wa Zimbabwe
Kamishna Msaidizi Paulo Nyathi amethibitisha kutokea kwa ajali na kwamba
watayataja majina ya wahanga wa tukio hilo baada ya uchunguzi kufanyika.
Mwanamke aliyenusurika
katika ajali hiyo Mollen Ngara ambaye alikuwa katika Basi la Govasburg ameviambia
vyombo vya habari kuwa uchovu wa dereva la Mandeep ndio uliomfanya aingie
kwenue upande waliokuwapo na kugongana uso kwa uso.
0 Comments:
Post a Comment