Tuesday, October 15, 2019

MAKTABA YA JAIZMELA: Balozi Isaac Abraham Sepetu ni nani?


Isaac Abraham Sepetu alizaliwa Oktoba 15, Mwaka 1943 huko Tabora, Tanganyika, lakini inatajwa kwamba wazazi wake walihamisha makazi yao kutoka Tabora na kuhamia kuishi visiwani Zanzibar, ambako hasa ndiko alipokulia na kusoma elimu ya msingi na sekondari, hii ilikuwa wakati Zanzibar ikiwa bado chini ya utawala wa kisultani.

Kwa hivyo kutokana na tamaduni na sheria za uraia wa Zanzibar, Isaac Sepetu akajikuta ni Mzanzibar ukizingatia pia uhuru wa nchi ya Zanzibar ulimkuta akiwa mkazi wa huko.

Balozi Isaac Abraham Sepetu alisoma elimu ya msingi na sekondari katika shule ya St. Joseph moja ya shule maarufu sana wakati huo, kwasasa ikijulikana kama "Skuli ya Tumekuja" iliyopo Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja hii ilikuwa kati ya mwaka 1952 - 1963.

Baada ya kutoka St. Joseph school, Isaac sepetu alikwenda moja kwa moja Berlin nchini Ujerumani, kujiunga na Chuo Kikuu cha Karl Max, sasa kinaitwa Leipzig University, Ujerumani ( Siku hizo ikifahamika kama Ujerumani mashariki), hii ilikuwa kati ya mwaka 1964 -1970 ambako alisomea fani mbali mbali ikiwemo Uandishi wa Habari, Uhusiano wa kimataifa na baadaye kuhitimu shahada katika siasa za Uchumi (degree in Political Economy).

Balozi Isaac Abraham Sepetu ni moja kati ya wasomi mahiri na bingwa wa kuzungumza kwa ufasaha lugha kubwa tatu adhimu za kimataifa, kikiwemo kiswahili, kiingereza na kijerumani. 

Sifa zingine za kipekee alizokuwa nazo ni pamoja na utulivu wa kiakili, mtu asiye na papara, mwingi wa hekima, busara na maarifa na hakika sifa hizi ndizo hasa zilizomsaidia sana kufanikiwa katika maisha kama mtumishi wa umma, Mwanasiasa na baba wa familia ya Mke na watoto wanne (wa kike) warembo akiwemo Bintie Wema Abraham Sepetu aliyepata kuwa mlimbwende wa Taifa mwaka 2006.

Isaac Abraham Sepetu alianza utumishi katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar mwanzoni mwa miaka ya 1970's Mara tu baada ya kurudi kutoka masomoni huko Ujerumani, ambapo alishika nyadhifa mbalimbali katika serikali ya Mapinduzi Zanzibar na baadae katika serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Baba wa Taifa na Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Mwalimu Julius kambarage Nyerere.

Balozi Isaac Abraham Sepetu alifariki asubuhi ya Oktoba 27, 2013, katika Hospitali ya TMJ Mikocheni, jijini Dar es Salaam, alikokuwa amelazwa akisumbuliwa na maradhi ya kiharusi pamoja na Kisukari.

0 Comments:

Post a Comment