Waziri Mkuu Kassim Majaliwa |
Serikali ya Jamhuri ya
Muuungano wa Tanzania imeondoa vikwazo vilivyokuwepo katika usafirishaji wa
sampuli za madini kutoka eneo moja kwenda eneo jingine.
Hayo yalijiri wakati wa
ufunguzi wa Maonyesho ya Pili ya Teknolojia na Uwekezaji katika Sekta ya Madini
kwa mwaka 2019 yatakayodumu kwa siku saba hadi Septemba 29 mwaka huu katika
viwanja vya CCM Kalangalala mkoani Geita.
Katika maonyesho hayo
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitangaza kuondoa vikwazo hivyo katika
usafirishaji wa sampuli hizo za madini ambapo hapo awali ulikuwa ukikabiliwa na
vikwazo mbalimbali.
Hapo awali ilikuwa ni
lazima kwa mujibu wa sheria kusafirisha sampuli hizo kwa ruhusa ya Kamishna wa
Madini au Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini
Hata hivyo Waziri Mkuu
aliwataka wamiliki wa leseni za usafirishaji na uyeyushaji wa madini kuzingatia
sheria, kanuni, taratibu na miongozo ili kunufaisha pande zote mbili, kulipa
kodi stahili na kuhakikisha leseni zao zinafanya kazi kwa muda uliopangwa.
Kwa upande wake
Mkurugenzi mtendaji wa Maabara ya Kupima
Sampuli za Madini nchini (SML), Mhandisi Simon Shinshi alisisitiza kuwa
wachimbaji wa madini wa wadogo wa kati
na wakubwa kuwa na taarifa sahihi za kimaabara pale wanapotaka kuchimba ili
kuwaongoza kwenye teknolojia na gharama.
Mhandisi Shinshi
aliongeza kuwa kwa kufanya hivyo itaondoa hasara kwani madini yatakuwa na
thamani stahili hivyo yatapandisha kwa kasi uchumi wa Tanzania.
“Wachimbaji wadogo
watumie maabara za ndani ambazo zinatoa majibu ya haraka na uhakika,” alisema
Mhandisi Shinshi.
Kwa mujibu wa taarifa
iliyotolewa na Maabara ya Madini nchini kwa mwaka 2018/19 wastani wa sampuli
50,000 ziliwafikia ikilinganisha na mwaka 2017/18 ambapo sampuli 40,000
zilifika katika maabara hali inayoonyesha kabla na baada ya vikwazo kuondolewa.
Aidha Mhandisi Shinshi
alifafanua kwamba hadi sasa wanayo matawi manane ya maabara kwenye maeneo
ambayo yanajihusisha na uchimbaji wa
madini hayo, huku akiyataja matawi hayo kuwa ni Mwanza, Geita, Katoro,
Kahama, Tarime, Singida, Chunya na Makongolosi.
Kifungu cha 18(2) cha
Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 kinakataza mtu yeyote zaidi ya mmiliki halali wa
leseni ya madini, kumiliki, kusafirisha au kuuza madini bila kuwa na kibali cha
kufanya hivyo kwa mujibu wa Sheria.
Kifungu cha 18(3) kinakataza mtu yeyote
kusafirisha nje ya nchi madini au sampuli za madini bila kuwa na leseni ya
madini, kibali cha kusafirisha madini nje ya nchi na uthibitisho wa malipo ya
mrabaha.
Kauli mbiu ya Maonyesho
ya Pili mwaka 2019 ni “Madini ni Chachu ya ukuaji wa Uchumi wa Viwanda,
tuwekeze kwenye teknolojia bora ya uzalishaji na tuyatumie masoko ya Madini.”
Imetayarishwa
na Kija Elias…………………….Septemba 29, 2019
0 Comments:
Post a Comment