Friday, October 25, 2019

Angola ni taifa la namna gani?



Angola ni taifa lililopo katika ukanda wa pwani-magharibi mwa Kusini-Kati ya Afrika. 

Angola ambalo ni taifa la saba kwa ukubwa barani Afrika likipakana na Namibia kwa upande wa kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa upande wa Kaskazini, Zambia kwa upande wa Mashariki na bahari ya Atlantiki kwa upande wa magharibi. Pia taifa hili lina jimbo moja la Cabinda ambalo limejishikiza katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Jamhuri ya Kongo. 

Mji mkuu wa Angola ni Luanda. Taifa hili limetawaliwa na Ureno tangu karne ya 16. Ilipofika karne ya 19 wahamiaji kutoka barani Ulaya walianza kuzama ndani zaidi katika taifa hilo. 

Mapema katika karne ya 20 ndipo mipaka rasmi ilichorwa  kutokana na upinzani wa Cuamato, jamii za Kwanyama na ile ya Mbunda. Taifa hili lina uchumi unaokua kwa kasi likiegemea katika uchimbaji wa madini na mafuta. Maisha ya watu nchini humo bado yapo chini huku umri wa kuishi ukiwa chini. 

Lina idadi ya kubwa ya watu wa Ovimbundu ambao wanachukua kiasi cha asilimia 39 ya idadi ya watu kwenye taifa hilo lenye takribani watu milioni 25.7. Jamii ya Ambundu inachukua asilimia 25 ya watu kwenye taifa hilo na na Bakongo wakichukua asilimia 13 ya watu. 

Uhuru wa taifa hilo ulipatikana Novemba 11, 1975. Hata hivyo baadaye ulikuja kuathiriwa kwa vita kali ya wenyewe kwa wenyewe iliyoongozwa na vyama vya MPLA na UNITA vilivyomalizika mwaka 2002. 

Katika vyama hivyo vilikuwa na mikono ya mataifa makubwa ya Urusi na Marekani. Vita hivyo vilimalizika baada ya kuuawa kwa kiongozi wa UNITA Jonas Savimbi. Savimbi aliuawa na vikosi vya serikali Februari 22, 2002 na kuzikwa siku iliyofuatia kwenye mkoa ulio mashariki wa Moxico. 

Wiki sita baadaye Unita walisaini makubaliana ya amani na serikali na kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka 27. 

UNITA kwanza waliendesha vita vya msituni dhidi ya utawala wa wareno kati ya mwaka 1966 na 1974 na kisha kikapigana na chama cha People's Movement for the Liberation of Angola (MPLA) wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe hadi wakati wa kifo cha Savimbi kwenye mapigano na vikosi vya serikali mwaka 2002. 

Watu wa taifa hilo wengi wao ni waumini wa Kikristo wa Kikatoliki. Lugha ya taifa hilo ni Kireno.

0 Comments:

Post a Comment