Tuesday, October 1, 2019

Ifahamu Kahawa ilivyoanza


Kitabu cha ALL ABOUT COFFEE kinaeleza hadithi ya Kahawa, kinasema  mmea huo inaanza katika maeneo ya milimani ya Ethiopia, mahali mmea wa mwituni wa kahawa unatoka. Mimea inayotokana nao, inayoitwa Coffea arabica, hutokeza theluthi mbili ya kahawa yote ulimwenguni. Hata hivyo, haijulikani kabisa ni wakati gani mambo yote kuhusu buni iliyokaangwa yalipojulikana. Ingawa hivyo, kahawa ya arabica ilikuwa ikikuzwa katika Peninsula ya Arabia kufikia karne ya 15 W.K. Licha ya kwamba kulikuwa na vikwazo vya kutoa mbegu za kahawa ambazo zingeweza kukuzwa kutoka huko, Waholanzi walipata miti au mbegu hizo mnamo 1616. Walisitawisha mashamba huko Ceylon, ambayo sasa ni Sri Lanka, na Java, ambayo sasa ni sehemu ya Indonesia.
Mnamo 1706, Waholanzi walisafirisha mti mchanga kutoka mashamba yao huko Java na kuupeleka kwenye mashamba fulani huko Amsterdam, Uholanzi. Mti huo ulinawiri. Mimea iliyotokana nao ilisafirishwa hadi koloni za Uholanzi huko Suriname na Karibea. Mnamo 1714, meya wa Amsterdam alimpa Mfalme Louis wa 14 wa Ufaransa mti mmoja. Mfalme aliagiza upandwe katika Jardin des Plantes, yaani, Bustani ya Kifalme huko Paris.
Wafaransa walitamani sana kuanza biashara ya kahawa. Walinunua mbegu na miti kisha wakaisafirisha hadi kisiwa cha Réunion. Mbegu zilishindwa kukua na watu fulani wanasema kwamba miti yote ilikufa isipokuwa mmoja tu. Hata hivyo, mbegu 15,000 kutoka kwenye mti huo mmoja zilipandwa mnamo 1720na mwishowe shamba la kahawa likaanzishwa. Miti hiyo ilionekana kuwa yenye thamani sana hivi kwamba mtu yeyote ambaye angepatikana akiiharibu angehukumiwa kifo! Pia Wafaransa walitaka kuanzisha mashamba huko Karibea lakini walishindwa walipojaribu mara mbili.

Ofisa Mfaransa wa kikosi cha majiniGabriel Mathieu de Clieu, alipokuwa likizoni huko Paris, alihakikisha kwamba amepeleka mti mmoja kwenye shamba lake aliporudi Martinique kutoka Ufaransa. Mnamo Mei 1723, alisafiri kwa meli kurudi kwenye kisiwa hicho akiwa na mti uliotokana na ule wa Paris.

Kitabu All About Coffee kinaeleza kwamba ili asafirishe mti huo, de Clieu aliutia ndani ya sanduku ambalo sehemu yake ilikuwa imetengenezwa kwa glasi ili ufyonze nuru ya jua na udumishe joto katika siku yenye mawingu. Msafiri mwenzake ambaye huenda alimwonea de Clieu wivu na ambaye hakutaka afanikiwe, alijaribu kumnyang’anya mmea huo lakini akashindwa. Pia uliokoka wakati meli hiyo iliposhambuliwa na maharamia wa Tunisia, ikapigwa na dhoruba kali, na hata kulipokuwa na upungufu wa maji safi wakati meli hiyo iliposhindwa kusonga kwa sababu ya kukosa upepo katika eneo la Ukanda Shwari. De Clieu aliandika hivi: “Maji yalikosekana kabisa hivi kwamba kwa zaidi ya mwezi mmoja nililazimika kugawa kiasi kidogo nilichopewa ili nimwagie mmea huo. Nilikuwa na matumaini makubwa kwamba ungefaulu nao ulikuwa chanzo cha furaha yangu.”

Jitihada za de Clieu hazikuwa za bure. Mmea huo ulifika Martinique ukiwa salama, nao ukanawiri na kuzaa sana katika mazingira hayo ya tropiki. “Kutokana na mmea huo mmoja, Martinique ilisambaza mbegu kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja katika nchi zote za Amerika isipokuwa Brazili, Guiana ya Ufaransa na Surinam[e],” anasema Gordon Wrigley katika kitabu chake Coffee.
Wakati huohuo, pia Brazili na Guiana ya Ufaransa zilitaka miti ya kahawa. Huko Suriname, Waholanzi walikuwa na mimea iliyotokana na ule wa Amsterdam lakini waliilinda kwa uangalifu. Hata hivyo, mnamo 1722, Guiana ya Ufaransa ilipata mbegu kutoka kwa mhalifu aliyekuwa ametoroka, akaingia Suriname na kuiba mbegu kadhaa. Serikali ya Guiana ya Ufaransa iliahidi kutomchukulia hatua na kumrudisha nchini iwapo angewapa mbegu hizo.
Jitihada za mwanzoni za kukuza mbegu au miche ya kahawa nchini Brazili hazikufua dafu. Kisha Suriname na Guiana ya Ufaransa zikawa na mzozo kuhusu mpaka nazo zikaomba Brazili iwape mpatanishi. Brazili ilimtuma ofisa wa jeshi anayeitwa Francisco de Melo Palheta, huko Guiana ya Ufaransa na kumwagiza asuluhishe mzozo huo nawakati huohuo arudi na mimea ya kahawa.
Kesi hiyo ilikuwa na mafanikio naye gavana akamfanyia Palheta karamu ya kumuaga. Ili kuonyesha uthamini wake kwa mgeni huyo wa heshima, mke wa gavana alimpa Palheta maua maridadi sana. Hata hivyo, katikati ya maua hayo kulikuwa na mbegu za kahawa ambazo zingeweza kukua pamoja na miche. Hivyo, inaweza kusemwa kwamba mnamo 1727, biashara ya kahawa ya Brazili inayoleta mabilioni ya dola ilianzia katikati ya maua.
Kwa hiyo, mti mdogo uliotoka Java kwenda Amsterdam mnamo 1706, na mimea ambayo ilienda Paris, ilitokeza kilichohitajika ili kupanda kahawa huko Amerika ya Kati na Kusini. Wrigley anaeleza hivi: “Kwa sababu hiyo msingi wote wa biashara ya kahawa ya arabicaulianzia mahali pamoja tu.”
Leo, zaidi ya mashamba milioni 25 yanayotunzwa na familia mbalimbali katika nchi 80 hivi hukuza miti bilioni 15 hivi ya kahawa. Vikombe bilioni 2.25 vya mazao yao hunywewa kila siku.
Kwa kushangaza, tatizo siku hizi ni kwamba kahawa hutokezwa sana. Hali imefanywa kuwa ngumu kwa sababu ya siasa, uchumi, na kwa sababu ya mashirika yenye nguvu kudhibiti masoko. Yote hayo yamewafanya wakulima wa kahawa katika nchi nyingi wawe maskini hohehahe. Hali hiyo inashangaza hasa unapofikiria miaka 300 hivi iliyopita jinsi de Clieu alivyogawa maji yake machache yenye thamani ili amwagie mojawapo ya miti hiyo.

AINA MBILI MAARUFU ZAIDI ZA KAHAWA
Jarida Scientific American linasema hivi: “Buni za kahawa ni mbegu za mmea wa jamii ya Rubiaceae, na kuna angalau aina 66 za mmea huo katika kundi linaloitwa Coffea. Aina mbili za kahawa inayouzwa sana ni Coffea arabica, ambayo ni thuluthi mbili ya kahawa yote inayokuzwa ulimwenguni, na C[offeacanephora, ambayo mara nyingi huitwa kahawa ya robusta, ambayo ni thuluthi moja ya kahawa yote inayokuzwa ulimwenguni.”

Kahawa ya robusta ina harufu nzito na mara nyingi husagwa na kuwa kahawa inayoweza kuyeyuka mara moja. Hata hivyo, mti huo unaweza kutokeza mazao mengi na hauathiriwi na magonjwa kwa urahisi. Mti huo hukua kufikia meta 12 hivi. Kimo hicho ni mara mbili ya mti wa arabica ambao haujakatwa matawi na ambao unaweza kuathiriwa upesi na ugonjwa nao hauzai sana. Buni ya robusta ina asilimia 2.8 ya kafeini hali buni ya arabicahaizidi asilimia 1.5 ya kafeini. Ingawa mti wa arabica una kromosomu 44 hali ule wa robusta na aina nyingine za kahawa za mwituni zina kromosomu 22, aina fulani zimefaulu kupandikizwa.

 “KUBATIZA” KAHAWA
Kahawa ilipopelekwa Ulaya kwa mara ya kwanza katika karne ya 17, makasisi fulani Wakatoliki waliiita kinywaji cha Shetani. Walifikiri kwamba ingechukua mahali pa divai, ambayo kwa maoni yao ilikuwa imetakaswa na Kristo. Hata hivyo, kitabu Coffee kinaeleza kuwa inasemekana kwamba Papa Clement wa Nane alionja kinywaji hicho na mara moja akabadili maoni yake kukihusu. Alisuluhisha tatizo hilo la kidini kwa kubatiza kinywaji hicho kwa njia ya mfano, na hivyo Wakatoliki wakaruhusiwa kunywa kahawa.

Jinsi Kahawa Ilivyoenea
1. Miaka ya 1400 “Arabica” yaanza kukuzwa kwenye Rasi ya Arabia
2. 1616 Waholanzi wapata miti ya kahawa au mbegu zinazoweza kupandwa
3. 1699 Waholanzi wapeleka miti huko Java na visiwa vingine huko East Indies
4. Miaka ya 1700 Kahawa inakuzwa huko Amerika ya Kati na Karibea
5. 1718 Wafaransa wapeleka kahawa Réunion
6. 1723 G. M. de Clieu apeleka mti wa kahawa kutoka Ufaransa hadi Martinique
7. Miaka ya 1800 Kahawa yaanza kukuzwa huko Hawaii 


0 Comments:

Post a Comment