Wednesday, October 2, 2019

MAKTABA YA JAIZMELA: Mahtma Gandhi ni nani?



Oktoba 2, 1869 alizaliwa mwanasheria, mwanafalsafa, mwanaharakati wa haki za binadamu na kiongozi wa siasa nchini India maarufu Mahtma Gandhi.

Gandhi alijulikana hasa kwa jina la Mahatma. Neno hili la Kisanskrit linamaanisha "roho kubwa". 

Aliitwa hivyo mara ya kwanza alipofika Bombay wakati wa kurudi kutoka Afrika Kusini. Gandhi hakupenda jina hilo lakini alishindwa kuzuia matumizi yake. Jina lake halisi ni Mohandas Karamchand Gandhi. 

Anajulikana hasa kama kiongozi wa harakati za uhuru wa Uhindi aliyepinga na kushinda ukoloni kwa njia ya amani bila ya matumizi wa mabavu au silaha. Gandhi alizaliwa katika eneo la Gujarat kama mtoto mdogo wa Karamchand Gandhi na mama Putali Bai. 

Baba yake alikuwa waziri mkuu katika serikali ya maharaja wa nchi lindwa ndogo ya Porbandar wakati ilipokuwa sehemu ya Uhindi wa Kiingereza. 

Familia yake ilifuata dini ya Uhindu, madhehebu ya Wavishnu, lakini nyumba ya Gandhi ilitembelewa pia na Waislamu na Wajain. Mwaka 1883 akiwa na umri wa miaka 13 aliozwa kwa mke wake Kasturba wakazaa watoto 4. 

Mwaka 1888 alisafiri kwenda Uingereza akasoma sheria kwenye chuo kikuu cha London, akapokewa kama wakili kwenye mahakama za juu kuanzia 1891. Huko Uingereza alisoma mengi juu ya Ukristo, akipendezwa hasa na mahubiri ya Yesu na hotuba ya mlimani, lakini hakuvutwa na nafasi ya pekee Yesu anayopewa katika imani ya Kikristo. 

Wakati uleule alianza kusoma vitabu vitakatifu vya Uhindu, hasa Bhagavad Gita iliyoendelea kuwa mwongozo wa kiroho maishani mwake. Baada ya mtihani alirudi Uhindi akafanya kazi kama wakili mjini Bombay. 

Mwaka 1893 alitumwa Afrika Kusini kwa kesi moja tu, lakini alibaki huko hadi 1914. Baada ya kuugua aliondoka Afrika Kusini mwaka 1914 akarudi Uhindi alipopokewa kama shujaa kwa sababu habari zake zilimtangulia. Aliunda makazi ya pamoja (ashram) alimoishi na watu waliofuata imani yake ya satyagraha. 

Alianza kuvaa nguo za wakulima wa kawaida. Ndani ya Uhindi yenyewe fitina ilianza juu ya nafasi ya Waislamu katika taifa jipya, huku sehemu kubwa ya Waislamu wakidai kugawiwa kwa koloni katika nchi mbili. Mapigano yalianza na watu elfu kadhaa waliuawa. 

Mnamo Agosti 1947 nchi mbili za India na Pakistan zilianzishwa, na Oktoba 1947 vita vikafuata kati ya nchi hizo mbili juu ya jimbo la Kashmir. Vita vikaongeza uadui, na watu milioni kadhaa walifukuzwa yaani Wahindu kutoka Pakistan na Waislamu kutoka India. 

Januari 30, 1948 Gandhi alipigwa risasi na kuuawa akitembea katika bustani ya nyumba huko Delhi. Mwuaji wake alikuwa Mhindu wa kundi lililofuata itikadi kali. Huyu kijana alikasirishwa na hatua za kupatanisha Waislamu na Wahindu akaamini Gandhi alikuwa msaliti wa Uhindu.

0 Comments:

Post a Comment