Thursday, October 17, 2019

Askari Polisi 3 wauawa Afrika Kusini, bendera zapepea nusu mlingoti




Bendera katika Jimbo la Cape ya Mashariki nchini Afrika Kusini zinapepea nusu mlingoti baada ya mauaji ya askari watatu ndani ya siku tatu ambao wameuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana. 

Ofisa wa Polisi mwenye umri wa miaka 47 ambaye amelitumikia jeshi la nchi hiyo kwa takribani miongo miwili alikutwa ameuawa ndani ya gari lake.

Msemaji wa Jeshi la Polisi Kanali Brenda Muridili amesema mwili wa Kapteni Mzikayise Kelemane ulikutwa karibu na barabara ya Addo mjini Port Elizabeth huku kukiwa na jeraha la risasi katika kichwa. 

Kanali Muridili ameongeza kuwa ofisa huyo wa jeshi alikuwa katika upelelezi wa kesi huko Port Elizabeth. 

Mke wa Kapteni Kelemane amesema alitoa taarifa za kutomuona mumewe katika kituo cha polisi siku moja kabla ya mwili wake kupatikana. 

Taarifa zinasema Kapteni Kalemane aliuawa Jumatatu ya Oktoba 14 mwaka huu. 

Aidha Kanali Muridili amesema Oktoba 1 mwaka huu ofisa wa kike wa jeshi naye alivamiwa na watu wasiojulikana  akiwa kwenye gari lake. 

Ofisa huyo wa kike amefahamika kwa jina la Sajenti Pathiswa Mhlola ambaye alikuwa akifanya kazi katika kituo cha Polisi cha Libode karibu na Umtata. 

Mauti yalimkuta akiwa na familia yake ndani ya gari walipozuiwa na gari jingine ambalo muuaji alianza kulimiminia gari lake risasi. 

Risasi hizo zilimpata katika eneo la juu la mwili wake katika kifua na tumbo ndipo alipokimbizwa hospitalini ambako aamefariki Oktoba 14 mwaka huu. 

Kanali Muridili amesema vifo hivyo viwili vimekuja baada ya kifo cha ofisa mwingine wa jeshi kilichotokea Jumamosi ya Oktoba 12 mwaka huu maeneo ya Umtata. 

Konstebo Thobani Sitolo mwenye umri wa miaka 34  akiwa nje ya majukumu ya kazi  alitandikwa risasi wakati akijaribu kupambana na watu waliokuwa wakiiba gari la rafiki yake. 

Ofisa huyo na rafiki yake walimkamata mwizi wao katika barabara ya Lewies huko huko Umtata ambapo alichomoa bastola na kuwatandika wote wawili lakini Konstebo Sitolo ambaye alikuwa akihudumu na jeshi hilo kwa muongo mmoja alipoteza maisha baada ya kufikishwa hospitalini. 

Polisi nchini humo inaendelea na uchunguzi juu ya matukio hayo.

CHANZO: THE SOWETAN

0 Comments:

Post a Comment