Tuesday, October 1, 2019

Malawi ni taifa la namna gani?



Malawi ni nchi iliyopo Kusini Mashariki mwa bara la Afrika ambayo zamani ilikuwa ikifahamika kwa jina la Nyasaland. 

Imepakana na Zambia kwa upande wa Kaskazini Magharibi, Tanzania kwa upande wa Kaskazini  Mashariki na upande wa Mashariki, Kusini na Magharibi inapakana na Msumbiji. 

Makadirio ya watu na makazi ya Julai 2016 yanaonyesha kuwa Malawi ina idadi ya takriani watu milioni 19. 

Sehemu kubwa ya eneo lake ni ziwa kubwa linaloitwa na majirani "Ziwa Nyasa" lakini nchini humo huliita "Ziwa Malawi". Pia kuna mzozo kati ya Malawi na Tanzania kuhusu eneo la ziwa ambao unazidi kufanyiwa kazi. 

Malawi ilikuwa na siasa ya chama kimoja chini ya rais wa kwanza Hastings Kamuzu Banda tangu kupata uhuru mwaka 1964 na masahihisho ya katiba 1966. Tangu kura ya wananchi mwaka 1993 Malawi imeanzisha mfumo wa vyama vingi vya kisiasa. 

Kutokana na katiba ya 1995 rais wa taifa anayechaguliwa na wananchi ndiye mkuu wa dola pia mkuu wa serikali. Makamu wa rais anachaguliwa pamoja naye lakini rais ana haki ya kumteua makamu wa pili asiyetoka katika chama chake. 

Mawaziri huteuliwa ama kati ya wabunge au nje ya bunge. Wabunge 193 wanachaguliwa moja kwa moja na wananchi kwa muda wa miaka mitano. Mahakama zinafuata mtindo wa Uingereza. Majaji huteuliwa kwa muda wa maisha; wanatakiwa kuwa huru na kutoathiriwa na siasa. 

Utawala hutekelezwa katika mikoa mitatu ya nchi zinazogawiwa katika wilaya 28. Wakuu wa mikoa na wilaya huteuliwa na serikali kuu. Mnamo Novemba 2000 kwa mara ya kwanza palifanyika uchaguzi wa ngazi ya chini mjini na vijijini. 

Serikali za mitaa zimeundwa na wilaya 28 katika maeneo matatu (Kaskazini, Kati na Kusini) yanayotawaliwa na Watawala wa Maeneo na Wakuu wa Wilaya ambao wanachaguliwa na serikali kuu. Chini ya ngazi ya wilaya kuna tarafa na vijiji vinavyoitwa maeneo madogo ya machifu. Uchaguzi wa kwanza wa Serikali za mitaa katika historia ya mfumo wa vyama vingi ulifanyika mnamo 21 Novemba 2000. 

UDF ilishinda asilimia 70 ya viti hivi katika uchaguzi huu. Wakazi wengi ni wa makabila ya Wabantu na wanatumia lugha za Kibantu, hasa Kichewa (57%), lakini lugha rasmi ni Kiingereza. 

Upande wa dini, wakazi wengi ni Wakristo (68-82%), wakifuatwa na Waislamu (13-25%). Rais wa taifa hilo kwa sasa ni Peter Mutharika.

Imetayarishwa na Jabir Johnson…….Oktoba 1, 2019.



0 Comments:

Post a Comment