Waandishi wa Habari mkoani Kilimanjaro Kija Elias, Rodrick Mushi, Venance Maleli, Profesa Bee, Enos Masanja |
Waandishi wa habari Mkoani Kilimanjaro, wamehamasishwa
kujiunga na vikundi vya Vicoba ili waweze kujikwamua kimaisha na kuboresha
maisha ya familia zao.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Moshi Tanzanite Vicoba
Group Maleli Venance, wakati wa hafla fupi ya kukabidhi kijiti hicho mara baada
ya kumaliza muda wake wa uongozi.
Venance alisema kuwepo kwa Vicoba ya waandishi wa
habari iliyoanzishwa mwaka 2013 umesaidia kuinua maisha ya wanahabari ambao
wameweza kujiunga pamoja na kuanzisha mfuko kwa jamii kwa ajili ya kuweka na
kukopa.
“Moshi Tanzanite Vicoba ni umoja unaoundwa na baadhi ya
wanahabari wa Mkoa wa Kilimanjaro, pamoja na akina mama lishe, uwepo wa kikoba
hiki umekuwa na manufaa makubwa sana kwetu sisi, hivyo tuwahamasishe na
wanahabari wengine ambao hawajaweza kujiunga kukitumia kikundi chetu kwa kuja
kujiunga nasi,”alisema Venance.
Aidha amewataka wanahabari hao kutumia fursa hiyo ili
kuongeza mitaji yao na kwamba kwa kufanya hivyo watakuwa na uelewa zaidi katika
masuala ya mnyororo wa thamani kwenye mazao, masoko ya kimataifa, fursa na
kuimarisha biashara.
Alisema kuanzishwa kwa Moshi Tanzanite Vicoba kumesaidia kwa
kiasi kikubwa kwa wanahabari kuwa na nidhamu ya fedha tofauti na hapo awali
ambapo mwandishi anapotoka kwenye majukumu yake ya kazi alikuwa akiitumia fedha
bila kuzalisha.
“Shughuli yoyote ya Maendeleo inahitaji mitaji hasa mitaji
ya fedha, kuanzishwa kwa Vicoba vya wanahabari kumesaidia kwa kiasi kikubwa
kujiletea maendeleo na kujikwamua kiuchumi,”alisema.
Kwa upande wake Mwenyekiti mpya wa kikundi hicho Fadhila
Omary , aliwashukuru wanachama hao kwa kumchagua kuwa mwenyekiti, ambapo
aliwaomba wanakikundi hao kumpa ushirikiano katika muda wote wa uongozi wake.
“Kuwepo kwa mfumo wa kuweka na kukopa kwa wananchama
waliojiunga kwa pamoja na kuunda kikundi kwa malengo ya kujikwamua na umasikini
(Vicoba), utawasaidia wanahabari walioko ndani ya kikundi hicho kukopa
kwa riba nafuu na pia itawawezesha wanahabari hao kukutana na kubadilishana
mawazo,”alisema Fadhila.
Katika uchaguzi huo Mwenyekiti alichaguliwa Fadhilla Omary,
Katibu Kija Elias, Mweka Hazina Charles Ndagulla, Mtunza nidhamu Upendo Mosha.
Wengine waliochaguliwa katika Moshi Tanzanite Vicoba yenye
wanachama 30 ni Queen Isack, Hellen Traiphone, Jackline Massawe, Deborah Nkya
na Winifrida Nyella.
Wakizungumza baadhi ya wanachama walionufaika na Vicoba
kupitia kikundi hicho cha Moshi Tanzanite Vicoba Queen Isack na Upendo Mosha,
walisema wameamua kuanzisha mradi wa ufugaji wa kuku ambao kwa sasa
zinawaingizia kipato na kuendesha shughuli za maisha yao.
Imeandikwa na Kija Elias, Moshi…………..Oktoba 14, 2019
0 Comments:
Post a Comment