Saturday, October 19, 2019

WanaCCM Mwanga Kilimanjaro wahofia kupoteza vijiji serikali za Mitaa

Baadhi ya wananchi wa CCM kijji cha Kileo wilayani Mwanga nje ya ofisi za CCM Mkoa wa Kilimanjaro.
Wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wa vijiji vya Kileo na Kituri wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro wameuonyoshea kidole cha lawama uongozi wa chama hicho ngazi ya wilaya kwa kuwateua wagombea wa nafasi za uenyekiti katika vijiji vyao kwa maslahi binafsi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wanachama hao wamesema kitendo cha kuteuwa wagombea ambao sio chaguo la wanachama kinaweza kupoteza nafasi na upinzani kuchukua uongozi wa vijiji vyao.

Wamesema walioteuliwa kuingia katika uchaguzi huo ambao unatarajiwa kufanyika kesho Oktoba 20 ni kwa maslahi yao binafsi na chuki miongoni mwa viongozi wa chama wa wilaya.

Mapema leo asubuhi wanachama hao waliwasili katika ofisi za chama mkoa wa Kilimanjaro kwa ajili ya kueleza masikitiko yao kutokana na viongozi wa wilaya kushindwa kuwasikiliza.

Hata hivyo maombi yao ya kusikilizwa yaligonga mwamba baada ya kumkosa Katibu Mkuu wa mkoa wa chama hicho kutokana na kuwa amesafiri kwa safari ya kiofisi.
Baadhi ya wananchi wa CCM kijji cha Kileo wilayani Mwanga wakitoka ofisi za CCM Mkoa wa Kilimanjaro.
Kwa upande wao wanachama hao wa Kituri wamesema wanayemhitaji ni Muhidin Samweli ambaye amekiongoza kijiji hicho kutoka mwaka 2010 hadi sasa lakini kinachoonekana jina lake limekatwa ili asionekane kabisa katika sanduku la kura.

Wamesema jina la mgombea Magala Abdallah Seushi hawalitaki hata kulisikia kwani alipokuwa mwenyekiti katika kipindi cha 2005-2010 alituhumiwa kwa kushindwa kumalizia zahanati na upotevu wa fedha

Aidha wanachama hao wamesema wanachotaka ni uchaguzi huo usimamishwe ili kutatua changamoto hiyo la sivyo italeta sintofahamu ikiwamo watu kutokwenda kupiga kura.

Hata hivyo Muhidin Samweli amedai kwamba licha ya jina lake kukatwa atabaki kuwa mwaminifu kwa Chama Cha Mapinduzi huku akisisitiza kuwa katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM wilayani hapo Salim Zuberi humo amekuwa mwiba mkubwa kutokana na maslahi yake binafsi.

Katibu wa CCM wilaya ya Mwanga Sixtus Mosha amesema hana muda wa kuzungumzia masuala hayo kwasababu amebanwa sana na majukumu. Hii sio mara ya kwanza kwa katibu huyo kushindwa kuzungumza na vyombo vya habari. Mosha alishawahi kufanya kazi za chama katika wilaya ya Hai, Siha, Moshi Mjini na sasa yupo katika wilaya ya Mwanga akitokea wilaya ya Rombo.

Imetayarishwa na Jabir Johnson……………………Oktoba 19, 2019

0 Comments:

Post a Comment