Tuesday, October 1, 2019

MAKTABA YA JAIZMELA: Jimmy Carter ni nani?


Oktoba 1, 1924 rais wa 39 wa Marekani Jimmy Carter. Jina lake halisi ni James Earl Carter Jr. 

Kiongozi huyo anafikisha miaka 95 hii leo na kuweka rekodi ya kuwa Rais wa kwanza kuishi muda mrefu baada ya kutoka madarakani katika historia ya marais wa taifa hilo. Jimmy Carter aliondoka madarakani akiwa na umri wa miaka 56. Aliiongoza Marekani kwa tiketi ya Chama cha Demokrati kuanzia mwaka 1977 hadi 1981. Kabla hajashika wadhifa wa kuwa Rais alikuwa Senata wa jimbo la Georgia katik ya mwaka 1963 hadi 1967. Mnamo mwaka 1971 alichaguliwa kuwa gavana wa 76 wa Georgia nafasi aliyodumu nayo mpaka 1975. Baada ya kumaliza kipindi chake cha urais Jimmy Carter alisalia katika sekta binafsi. Mnamo mwaka 2002 alitunukiwa tuzo ya Amani ya Nobel kutokana na mchango wake kupitia Carter Center. Alizaliwa na kukulia huko Plains katika jimbo la Georgia. Alihitimu masomo yake mwaka 1946 katika masuala ya Jeshi la Majini. Baada ya kifo cha baba yake mwaka 1953 Carter aliachana na masuala ya jeshi na kurudi nyumbani Georgia ambako alijishughulisha na masuala ya kulea familia na kilimo biashara cha karanga. Carter alizaliwa katika hospitali ambako mama yake alikuwa ni Nesi. Hadi sasa Carter yupo na mkewe Rosalynn mwenye umri wa miaka 73 wakiishi katika eneo alilozaliwa mji wenye watu 700 wa Plains. Tangu utoto wake alikuwa ni wa kujituma katika kazi. Akiwa na miaka 10 kuuza kile ambacho walikuwa wakizalisha kutoka shamba la familia, ambapo miaka mitatu baadaye alifanikiwa kupata akiba ambayo ilimfanya anunue nyumba tano kwa bei rahisi na kuanza kupangisha. Jimmy Carter ndiye rais pekee wa Marekani aliyehitimu mafunzo ya jeshi la majini na kuwa ofisa wa jeshi wa Submarines. Nafasi ambayo alidumu nayo kwa miaka saba. Jimmy Carter alichukua nafasi ya Urais wa taifa hiyo baada ya kumwangusha mgombea wa Republican Gerald Ford. Wakati wa utawala wake aliwekea mkazo program mbalimbali za elimu na ulinzi wa mazingira pia masuala ya haki za binadamu. Hata hivyo Carter alikutana na vikwazo vingi  ikiwamo matatizo katika ukuaji wa uchumi wa taifa hilo hususani katika masuala ya nishati ambako kulishuhudiwa misururu mirefu ya watu wakipanga foleni kwa ajili ya kununua nishati ya gesi. Atakumbukwa kwa kusuluhisha mgogoro wa Misri na Israel. Alianguka katika uchaguzi kutokana na kushindwa kuwaokoa mateka 52 wa Marekani waliokuwa wakishikiliwa nchini Iran zaidi ya mwaka mmoja. Baada ya kuondoka katika nafasi hiyo Carter kama ilivyokuwa kwa baba yake alikuwa akifundisha masomo ya Jumapili kanisani mara mbili kila mwezi kwenye Kanisa la Baptist mjini Plains ambapo kitendo hicho kilikuwa kikiwavuta wengi kutokana maeneo mbalimbali kwenda kumsikiliza.

0 Comments:

Post a Comment