Serikali imesema matumizi
makubwa ya fedha imekuwa ikifanya katika ununuzi wa madawa tiba kwa magonjwa ya
milipuko yanayosababishwa na wananchi kula chakula bila kunawa mikono na
sabuni.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro
Dkt. Anna Mghwira aliyasema hayo jana katika siku ya unawaji mikono Duniani,
ambapo huadhimishwa Oktoba 15 kila mwaka ambapo mkoani Kilimanjaro ilifanyika
katika Shule ya Msingi Kiboroloni iliyopo Manispaa ya Moshi.
Kwa niaba ya Mkuu wa mkoa,
Afisa afya na Usafi wa Mazingira mkoa wa Kilimanjaro Jonas Mcharo, alisema kama
Taifa ni muhimu kuwekeza nguvu katika kuelimisha jamii hasa umuhimu wa kunawa
mikono kwa maji safi na sabuni ili kujenga Taifa lenye afya bora ambalo
litakuwa na watu wenye afya bora.
“Siku ya unawaji mikono
huadhimishwa kila Oktoba 15 ya kila mwaka Duniani kote kwa Tanzania tulianza
kuadhimisha mwaka 2011, lengo likiwa ni kuhamasisha jamii kujenga uelewa juu ya
umuhimu wa unawaji mikono ili kuweza kupunguza magonjwa yanayoweza kuambukizwa
kwa mikono iliyochafuliwa kama vile mafua, kuhara, kuhara damu, udumavu minyoo
na homa ya mapafu,” alisema Mcharo.
Alisema kauli mbiu ya
maadhimisho hayo mwaka huu ni ‘Clean Hands For All” ambayo yanaikumbusha jamii
kuona umuhimu wa kunawa mikono na sabuni ili kujikinga na maradhi yatokanayo na
uchafu.
Mcharo amewataka wananchi
kuunga mkono juhudi za usafi kwa kunawa mikono na sabuni ili kujikinga na
maradhi yatokanayo na uchafu ili kuepusha taifa kutumia fedha nyingi kwenye
ununuzi wa madawa tiba kwa magonjwa ambayo yanaweza kuepukika.
Alisema hali ya unawaji
mikono katika Bara la Afrika siyo ya kuridhisha kwani nchi nyingi zina wastani
wa chini ya asilimia 50 na kwa Tanzania ni asilimia 12 tu ya kaya zenye vifaa
vya kunawia mikono vinavyofanya kazi.
“Bado kuna tatizo kubwa
sana la watu kutokunawa mikono, asilimia 70 hadi 80 ya wagonjwa tunaowapokea
katika hospitali zetu pindi wanapochunguzwa na madaktari wanagundulika kuwa na
ugonjwa unaotokana na uchafu,”alisema Mcharo.
Aidha alisema takwimu
zinaonyesha kuwa katika Mkoa wa
Kilimanjaro ni asilimia 66% ya kaya
hazina vifaa vya kunawia mikono, huku asilimia 34 pekee ndiyo ina vifaa vya kunawia mikono, ambapo asilimia 98 ya kaya zina vyoo.
Mcharo aliongeza kusema
kuwa “Endapo jamii itajenga tabia ya kunawa mikono ni dhahiri kuwa tutaweza
kuwafundisha pia watoto wetu ustaarabu na umuhimu wa kunawa mikono kwa kutumia
sabuni na maji tiririka.
Kwa upande wake Meneja
Miradi wa asasi isiyo ya kiserikali ya Childreach Tanzania Winfrida Kway,
alisema asasi hiyo ambayo imejikita
katika kuchangia uboreshaji wa upatikanaji wa huduma za elimu, afya, haki za
mtoto pamoja na ulinzi na usalama wa mtoto kwa kushirikiana na serikali.
Winfrida alisema katika
kipindi cha mwaka 2017/2018 Childreach
Tanzania, imeweza kutekeleza miradi saba kwa jamii ukiwemo mradi wa ukarabati
wa jiko la shule ya msingi Sango, uchimbaji wa kisima cha maji shule ya msingi
Njiapanda walemavu, mradi wa Shule yangu Suti Yangu ambao ulitekelezwa katika
shule ya msingi Mkomilo.
Aidha aliitaja miradi
mingine kuwa ni mradi wa mafunzo kwa vitendo, unaotekelezwa kwa kushirikiana na
Chuo cha ufundi Stadi cha viziwi Ghona, mradi wa Maisha Bora ambao unatekelezwa
katika mikoa ya Arusha na Manyara, mradi wa elimu, afya na mazingira na mradi
wa Sholarship ambao unafadhili gharama za elimu za watoto wanaoishi katika
mazingira magumu.
Winfrida aliongeza kuwa Childreach Tanzania, kwa mkoa wa Kilimanjaro
imeweza kuzifikia shule za msingi takribani 23 zenye wanufaika 13, 357 ambapo
kati ya hao 6,847 ni watoto wa kiume na 6,510 ni watoto wa kike ndani ya wilaya
ya Moshi mjini na vijijini.
“Kupitia mradi wa unawaji
mikono Childreach Tanzania, imeweza
kukarabati na kujenga miundo mbinu ya shule 26 za msingi ikiwemo vyoo, mambomba
ya maji taka, sehemu maalumu za kunawia mikono ambazo zinaweza kuhudumia watoto
30,” alisema.
Shirika la Watoto Duniani
UNICEF mwaka 2018 lilibaini kuwa asilimia 63 ya shule za msingi zilizoko Tanzania Bara ndio zinahuduma
maalumu za unawaji wa mikono huku
asilimia 42 ya shule za msingi bado hazina kabisa huduma ya unawaji wa mikono.
Wanafunzi wa Sule ya Msingi Kiboroloni na Mnazi zote za Mjini Moshi wakionyesha kwa vitendo namna ya kunawa mikono katika Siku ya Kimataifa ya Kunawa Mikono inayofanyika Oktoba 15 kila mwaka. |
Imetayarishwa na Kija Elias…..Oktoba
15,2019. Imehaririwa na Jabir Johnson
0 Comments:
Post a Comment