Tuesday, October 15, 2019

Wananchi Kilimanjaro wafunguka kasi ndogo uandikishaji kura Mitaa

Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro Dkt. Anna Mghwira akizungumza na Wafanyabiashara wa Soko la Kiboroloni mjini Moshi Okt 15 mwaka huu.

Wananchi mkoani Kilimanjaro wameweka bayana vikwazo ambavyo vinasababisha kasi ndogo uandikishaji wa kupiga kura katika serikali za mitaa kuwa na kasi ndogo mkoani humo.

Hayo yanajiri baada ya takwimu za Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuweka bayana kuwa mikoa ya Dar es Salaam, Kilimanjaro na Arusha imekuwa nyuma katika zoezi la kujiandikisha kupiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 24 mwaka huu.

Wakizungumza mbele ya mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Dkt. Anna Mghwira katika ziara ya kuhamasisha uandikishaji wa upigaji kura aliyoifanya katika masoko ya mjini Moshi Oktoba 15 mwaka huu wamesema shughuli zao za biashara zimekuwa zikiwabana hadi kusababisha kukosekana kwa muda wa kwenda kujiandikisha katika mitaa ambayo wanayoishi.

Aidha wananchi hao hawakusita kuweka bayana kuwa elimu kuhusu kujiandikisha kwa ajili ya uchaguzi wa Novemba 24 haikutolewa ipasavyo huenda ni kutokana na makosa yao binafsi ambayo yalitokana na kushindwa kupata nafasi ya kwenda katika vituo.

Pia katika ziara hiyo wananchi wamelitaja baadhi ya changamoto zinazowakabili katika maeneo wanayoishi ambayo kwa kiasi kikubwa yamekuwa yakiwakatisha tamaa kujiandikisha kwa ajili ya upigaji wa kura uchaguzi serikali za mitaa mwaka huu.

Wananchi wa Njiapanda walisema mabasi ya mikoani yamekuwa yakikataa kusimama katika kituo cha mabasi cha Njiapanda hata kama yanalipa ushuru wa stendi hiyo lakini yamesababisha maduka mengi kufungwa kutokana na kukosa wateja na biashara kuwa ngumu.

“Juhudi za serikali zimekuwa muhimu kwetu na tumekuwa tukiziona lakini katika hili la stendi ya Njiapanda kwa kweli limetukatisha tamaa, tumekuwa tukipeleka kilio chetu lakini hakifanyiwi kazi sasa tutapata moyo wapi wa kujiandikisha kupiga kura?” alisema mfanyabiashara mmoja wa Njiapanda.

Hata hivyo wameishukuru Serikali kwa kuwaongezea siku za kujiandikisha kupiga kura na kwamba kilichokua kikiwachanganya ni vitambulisho walivyopata katika uandikishaji wa kupiga kura uchaguzi mkuu 2020 wa Rais, Wabunge na Madiwani ambao wana vitambulisho.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa Dkt. Mghwira amesema ni kweli Kilimanjaro imekuwa miongoni mwa mikoa ambayo uandikishwaji kwa ajili ya kupiga kura umekuwa ukienda kwa kasi ndogo.

Ziara hiyo ya Wilayani Moshi mkoani humo imewagusa wafanyabiashara wa masokoni katika maeneo ya Memorial, Mbuyuni, Manyema, Soko Kuu la Kati, Kiboroloni na Njiapanda.

Imetayarishwa na Jabir Johnson…..Oktoba 15, 2019

0 Comments:

Post a Comment