Tuesday, October 22, 2019

Msumbiji ni taifa la namna gani?


Taifa hili lipo upande wa Kusini Mashariki wa Afrika likipakana na Bahari ya Hindi kwa upande wa Mashariki. 

Linapakana na Tanzania kwa upande wa Kaskazini, Malawi na Zambia kwa upande wa Kaskazini Magharibi, Zimbabwe kwa upande wa Magharibi na Eswatini na Afrika Kusini kwa upande wa Kusini Magharibi. 

Pia Msumbiji imetanganishwa na pwani ya bahari ya Hindi ili kuvifikia visiwa vya Comoro, Mayotte na Madagscar. 

Mji mkuu wa Msumbiji ni Maputo ambao ulibadilishwa mwaka 1976 hapo awali tangu mwaka 1876 ulikuwa ukifahamika kwa jina la Lourenco Marques. Katika karne ya kwanza na ya tano A.D; jamii ya wabantu ilihamia katika eneo hilo ambalo kwa sasa ndio Msumbiji  wakitokea Kaskazini ya Mbali na Magharibi. 

Msumbiji ya Kaskazini ilikuwa ikikabiliwa na zile pep za Kusi na Kasi maarufu Monsoon kutoka Bahari ya Hindi. 

Kati ya karne ya 7 hadi 11 miji ya Kiswahili katika pwani ya Msumbiji ilianza kupatikana kutokana na ujio wa wageni hao ambao walianza taratibu kuwa wengi hata kufikia kuwa na utamaduni wa Kiswahili ikiwamo lugha yao. 

Katika karne za katikati kulikuwapo mwingiliano wa watu wa kibiashara na Somalia, Ethiopia, Misri, Uarabuni, Uajemi na India. Mnamo mwaka 1498 ujio wa msafara wa Mreno Vasco da Gama ulifanya Wareno kuanza kuishi hapo. Makazi rasmi ya wareno nchini Msumbiji yalianza mwaka 1505. 

Baada ya karne nne Msumbiji ilijipatia uhuru wake kutoka kwa Wareno, hiyo ilikuwa mwaka 1975 chini ya uongozi wake Samora Machel ambaye hakudumu sana katika nafasi hiyo ya uongozi kwani aliuawa. 

Miaka miwili baada ya uhuru huo Msumbiji waliingia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vilianza mwaka 1977 hadi 1992. Mnamo mwaka 1994, Msumbiji ilifanya uchaguzi wake wa kwanza wa vyama vingi licha ya kutokuwa imara. 

Msumbiji ni taifa tajiri likijikita katika kilimo, Utalii na uchimbaji wa madini hususani aluminium na mafuta. Msumbiji imekuwa ikifanya biashara zake moja kwa moja na mataifa kama Brazil, Ubelgiji, Ureno na Hispania. 

Tangu mwaka 2001  Thamani ya pato la mwisho litokanalo na bidhaa au huduma fulani katika mwaka (GDP) ilionyesha kuwa Msumbiji ipo juu. Licha ya GDP kuonyesha kuwa nzuri na ya juu bado Msumbiji inaonekana kuwa ni nchi maskini na ikiwa katika ukanda wa chini kabisa wa nchi zinazoendelea. 

Nusu ya idadi ya watu nchini Msumbiji wanazungumza Kireno. Huku wengine wakizungumza lugha za kienyeji Makhuwa, Sena na Kiswahili. Idadi kubwa ya watu akali ya milioni 29 katika taifa hilo ni Wabantu. Rais wa sasa wa taifa hilo ni Filipe Nyusi.

Imetayarishwa na Jabir Johnson……………………………..Oktoba 22, 2019

0 Comments:

Post a Comment