Friday, October 4, 2019

MAKTABA YA JAIZMELA: Rutherford B. Hayes ni nani?


Oktoba 4, 1822 alizaliwa Rais wa 19 wa Marekani Rutherford Birchard Hayes. Mwanasiasa huyo kwa tiketi ya chama cha Republican aliiongoza Marekani mwaka 1877 hadi 1881. 

Alijiunga na Republican mwaka 1854 akitokea chama cha Whig. Aliwahi kuwa seneta na gavana wa jimbo la Ohio. Alizaliwa Delaware, Ohio kwa wazazi Rutherford Hayes Jr na Sophia  Birchard. Baba yake alikuwa mtunza stoo mjini Vermont. Ilipofika mwaka 1817 alihamia Ohio. Baba yake alifariki dunia majuma machache baada ya kuzaliwa kwa Rutherford. Mama yake alichukua nafasi ya kuitunza familia hiyo. Wawili kati ya wanne tu ndio waliojaliwa kufikia ukubwani ambaye ni Rutherford na dada yake Fanny wengine wawili walifariki dunia wakiwa bado wadogo. Asili ya Rutherford ni kutoka kwa wahamiaji kutoka Scotland ambao walihamia nchini Marekani mwaka 1625. Babu yake mzee Ezekiel alipigana vita vya Mapinduzi nchini Marekani maarufu American Revolutionary War akiwa katika cheo cha Captain huko Connecticut. Rutherford alisomea sheria na enzi za utawala wake alikuwa mstari wa mbele kuwatetea wakimbizi waliokuwa wafungwa na mpambano yake dhidi ya biashara ya utumwa. Alikuwa mpatanishi wa makundi yaliyokuwa yamegawanyika baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe katika ardhi hiyo. Mnamo mwaka 1876 alichaguliwa na wajumbe wa Republican kupeperusha bendera katika nafasi ya Urais na kuweka rekodi ya kuwa miongoni mwa marais wa Marekani waliochaguliwa kwa mchuano mkali wa kura. Hayes alimpoteza mgombea wa Urais maarufu kwa tiketi ya Chama cha Demokrati Samuel J. Tilden. Kura 20 za Wabunge wa Congress ziliongezwa na kumfanya Hayes kupita kwa ushindi mwembamba kwani bila hivyo Demokrati walikuwa mbele kwa kila kitu. Baada ya kipindi cha kwanza kumalizika Hayes aliwaomba wajumbe wa Republican asiendelee katika kipindi cha pili hivyo alistaafu na kurudi zake Ohio ambako alisaliwa kuwa wakili wa masuala ya kijamii na elimu. Mwandishi wa Historia Ari Hoogenboom alimwelezea Hayes kuwa maendeleo yake makubwa ni pale aliporudisha imani kwa wananchi kwa Rais baada ya mauaji ya Abraham Lincoln. Japokuwa waungaji mkono wake walikuwa wakimsifu kwa kurudisha Huduma za Umma wanahistoria na wasomi wamekuwa wakimchukulia kama kiongozi wa wastani.

0 Comments:

Post a Comment