Oktoba 5, 1952 alizaliwa
Waziri Mkuu wa sasa wa Pakistan Imran Khan. Jina lake halisi ni Imran Ahmed
Khan Niazi.
Ameweka rekodi ya kuwa Waziri Mkuu wa 22 wa taifa hilo lililopo
barani Asia. Kabla ya kuingia katika masuala ya siasa Khan alikuwa mchezaji wa
kimataifa wa Kriketi. Miongoni mwa mafanikio makubwa katika mchezo huo ni pale
alipoiongoza timu ya taifa kutwaa Kombe la Dunia la Kriketi mnamo mwaka 1992. Ushindi
huo ulikuwa wa kwanza na wa pekee katika taifa la Pakistan. Fainali ya kriketi
ilichezwa jijini Melbourne, Australia ambapo Pakistan chini ya unahodha wake
Imran Khan iliwazabua England kwa mikimbio 22. Hiyo ilikuwa Machi 25, 1992
mbele ya watazamaji 87,182. Khan alistaafu baada ya kutwaa taji hilo la dunia
akiwa na rekodi ya mikimbio 3,807 na wiketi 362 katika mashindano mbalimbali
aliyocheza. Aidha Khan anasalia kuwa miongoni mwa nyota wa nane waliofanya
vizuri katika All Rounders ikiwa na maana rekodi katika kuviringisha mipira na
kupiga. Na mwaka 2010 alikuwa miongoni ya watu maarufu walioingizwa katika
Kumbukumbu za Wakongwe wa Kriketi za Shirikisho la Kriketi Duniani (Hall of
Fame). Imran Khan alizaliwa mjini Lahore, na kupata elimu yake katika chuo cha
Aitchson kilichopo Lahore. Pia akaendelea katika Shule ya Royal Grammar
Worcester nchini England. Khan hakuishia hapo alisoma katika chuo cha Kebler
kikiwa ni tawi la Chuo Kikuu cha Oxford nchini England.. Alianza kucheza
kriketi akiwa na umri wa miaka 13 na kwa mara ya kwanza akiwa na umri wa miaka
18 aliitwa katika timu ya taifa ya Pakistan. Mchezo wake wa kwanza ulikuwa
mwaka 1971 katika Test Series dhidi ya England. Baada ya kuhitimu masomo yake huko
Oxford rasmi alianza kuitumikia Pakistan mwaka 1976 hadi alipostaafu mwaka
1992. Alipata kitambaa cha unahodha mwaka 1982 hadi alipostaafu. Mnamo Aprili
1996 Khan alianzisha chama cha siasa ambacho kwa sasa ndiye mwenyekiti cha
Tehreek-e-Insaf kikiwa ni chama cha mrengo wa kati. Miongoni mwa mafanikio
makubwa ya chama hicho ni kuunda serikali ya muungano katika jimbo la Kaskazini
Magharibi la Khyber Pakhtunkhwa. Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2018
Tehreek-e-Insaf kilifanikiwa kutwaa ushindi wa kishindo katika viti bungeni dhidi
ya chama tawala PML; hatua ambayo ilimweka madarakani Imran Khan katika serikali
ya shirikisho. Khan anasalia kuwa mtu maarufu katika ardhi ya Pakistan. Pia
Imran Khan ameandika kitabu cha ‘Pakistan: A Personal History’.
0 Comments:
Post a Comment