Ufalme wa Eswatini ni jina
ambalo limeanza kutumika mwaka 2018, hapo awali ilikuwa ikifahamika kwa jina la
Swaziland.
Ni taifa dogo sana Kusini mwa Afrika ambalo limejifunga. Kutoka
upande wa mashariki hadi magharibi ni umbali wa kilometa 130 na Kaskazini hadi
kusini ni umbali wa zaidi ya kilometa 200.
Eswatini ni nchi ndogo kuliko zote Kusini
mwa Afrika, ikiwa imeundwa na milima na baridi na maeneo baadhi yenye joto na
ukame. Lugha asili ya taifa hilo ni siSwati.
Ufalme huu ulianza rasmi
kutambuliwa baada ya uwepo wa uongozi imara wa Ngwane III. Eswatini inapakana na Afrika Kusini na Msumbiji.
Majina yanayotumika
sasa kwa kiasi kikubwa yametokana na uongozi wa Mswati II aliyeongoza mapambano
makali hadi mipaka ikachorwa miaka 1881.
Baada ya Vita ya Pili ya Makaburu iliyoanza
1899 na kumalizika mwaka 1902, Eswatini ilipewa jina la Swaziland ikiwa
mikononi mwa Waingereza. Septemba 6, 1968 ilijipatia uhuru wake.
Katiba
inayotumika sasa ya taifa hilo ni ya mwaka 2005. Mfumo wa utawala ni wa kijadi
unaoongozwa na Ngwenyama ambaye ni Mfalme Mswati III na Ndlovukati ambaye ni
Malkia Ntfombi Tfwala tangu mwaka 1986.
Uchumi
wa taifa hilo ni mdogo mno ikiwa ni miongoni mwa mataifa yanayoendelea. Kwa
makadirio ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2016 inaonyesha taifa hilo lina
takkribani watu milioni 1.3
Eswatini ina changamoto kubwa ya maradhi ya HIV/AIDS
na kifua kikuu. Inakadiriwa asilimia 26 ya watu wameathiriwa na virusi vya
ukimwi. Umri wa kuishi wa watu wa taifa hilo ni miaka 58.
Idadi kubwa ya watu
katika Eswatini ni vijana walio na wastani wa umri wa miaka 20.5 ambao
wanachangia asilimia 37.5 ya watu katika taifa hilo.
Imetayarishwa
na Jabir Johnson…….Oktoba 21, 2019
0 Comments:
Post a Comment