Wednesday, October 30, 2019

Komoro ni taifa la namna gani?


Komoro ni taifa huru kwenye funguvisiwa katika Bahari Hindi upande wa Mashariki wa Afrika. 

Iko katika Kanali ya Msumbiji kaskazini kwa Madagaska na mashariki kwa Msumbiji. Jina limetokana na lugha ya Kiarabu ambapo Juzur al-Qamar likiwa na maaana ya "visiwa vya mwezi". 

Komoro ina visiwa vitatu vikubwa: Grande Comore (Ngazidja), Anjouan (Nzwani) na Moheli (Mwali). Kisiwa cha Mayotte ni sehemu ya funguvisiwa kijiografia lakini kisiasa ni sehemu ya Ufaransa kwa sababu wakati wa kupata uhuru watu wa Mayotte walitamka kwa kura nyingi (73%) ya kwamba wanataka kukaa na Ufaransa. 

Lakini Komori inadai ni sehemu ya eneo lake. Komoro ni sehemu ya bara la Afrika. Ina pia visiwa mbalimbali vidogo. Hali ya hewa ni ya kitropiki. Kuna mvua miezi yote. Kitovu cha kisiwa kikubwa zaidi (Grande Comoro) ni mlima wa volkano hai Karthala wenye mita 2,461 juu ya Usawa wa Bahari. 

Volkano hiyo ya Karthala ililipuka mwaka 1977 ikaharibu kijiji kimoja. Visiwa vya Komoro vimekaliwa na watu mbalimbali kutoka Afrika na Asia Kusini katika historia ndefu. Wanaakiolojia walitambua mabaki ya makazi ya watu kutoka karne ya 6 kwenye kisiwa cha Nzwani lakini haijulikani kama watu walitangulia kufika mapema bila kuacha mabaki ya kutambulika. 

Waswahili wa kwanza walifika kama sehemu ya uenezi wa Wabantu tangu karne ya 9 BK. Kipindi cha kwanza huitwa kipindi cha Dembeni (karne ya 9 - 10) ambako Waswahili walianzisha kijiji kimoja katika kila kisiwa. 

Wakati wa karne ya 11 hadi ya 15 biashara iliongezeka na Madagaska pia na wafanyabiashara kutoka Uarabuni. Vijiji vidogo vikaongezeka na vijiji vya awali vikakua vikawa miji. Kumbukumbu ya wenyeji hutaja mara nyingi majina ya Waarabu kutoka Yemen na Saba' kama mababu wa koo asilia lakini hakuna uhakika kama kumbukumbu hizo zinalingana na historia halisi. 

Kufuatana na katiba ya uhuru ya mwaka 1975 Komori ilitangazwa kuwa jamhuri ya Kiislamu. Serikali zilipinduliwa mara kwa mara na wanajeshi au na mamluki. 

Katiba mpya ya mwaka 2001 imeondoa tabia ya kidini ya dola na iliunda utaratibu wa urais kuzunguka kati ya visiwa vitatu vikubwa. Katika muundo huo rais wa jamhuri atateuliwa kila baada ya miaka minne kutoka kisiwa tofauti. Katika uchaguzi wa 2010 ndiye Ikililou Dhoinine aliyepata kura nyingi. 

Watu wa Komori ni mchanganyiko wa Waarabu, Wamadagaska, Waafrika wa bara ambao mababu walikuwa watumwa, Wahindi na Wazungu kadhaa. Kutokana na uhaba wa ajira Wakomori wengi wamehamia nje, hasa Madagaska. 

Wakazi wengi ni Waislamu (98%, hasa Wasunni), wakifuatwa na Wakristo (2%). Karibu nusu ya wananchi wote hawajui kusoma. 

Ina lugha rasmi tatu ambazo ni Kifaransa, Shikomor (inayofanana na Kiswahili) na Kiarabu. 

Nje ya Kifaransa, Kiarabu na Kimalagasi Sanifu, kuna lugha tatu za asili ambazo huzungumzwa na Wakomori, yaani Kimwali, Kindzwani na Kingazidja ambazo ziko karibu na Kiswahili. 

Komoro ni kati ya nchi maskini zaidi duniani. Kilimo, uvuvi, uwindaji na misitu ni misingi ya uchumi wote.

0 Comments:

Post a Comment