Thursday, October 31, 2019

Ushelisheli yatoa wito kwa mataifa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa


Rais Danny Faure wa Ushelisheli; nchi isiyozidi watu 100,000

Rais Danny Faure wa Ushelisheli amesema hakuna muda wa kutupiana lawama katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa. 

Taarifa ya Ikulu ya Ushelisheli imesema ni vema kuacha kurushiana lawama kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa.  

Faure amesema sayansi ipo sawa katika hilo, wanasayansi wameshazungumza  kuhusu tatizo hilo na kwamba kinachotakiwa ni hatua za kimataifa katika kupambana na hilo na sio kunyosheana vidole vya lawama.

Faure amesema uchafuzi wa maji katika bahari umekuwa wa kiwango cha juu kwani Kilogramu 25,750 za plastiki zimekusanywa kutoka bahari hali inayoonyesha kuathirika kwa bahari. 

Uchafuzi wa maji katika bahari hiyo umesababisha kupanda kwa joto linalosababisha miamba kulika. Taifa hilo la Ushelisheli linaendelea na kampeni ya kutunza maji yake na kwamba theluthi moja ya maji yanatarajiwa kulindwa mwaka ujao katika mpango kazi huo. 

Wanasayansi wanatarajia kutoa ripoti yao kuhusu utafiti wao katika kilele cha Mkutano wa Mabadiliko Tabia Nchi wa mataifa yaliyoko katika Bahari ya Hindi mnamo mwaka 2022 utakaofanyika nchini humo.

CHANZO: SEYCHELLES NATION

0 Comments:

Post a Comment