Wednesday, October 30, 2019

Chadema Kilimanjaro walia rafu uchukuaji wa fomu serikali za mitaa


Chama cha Demokrasia na Maendeleo  (CHADEMA) mkoa wa Kilimanjaro kimewanyoshea kidole cha lawama wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi wa serikali za mitaa katika kipindi hiki ambacho wagombea mbalimbali za nafasi katika mitaa wakichukua na kurudisha fomu.

Hayo yanajiri ikiwa ni siku moja tangu kupulizwa kwa kipenga cha uchukuaji wa fomu za kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika mitaa zilizotangazwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo.

Katibu Mkuu wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro Basil Lema amesema kuna dosari katika maeneo ya Makuyuni na Mandaka ambapo Maafisa Watendaji ambao ni Wasimamizi wa Uchaguzi huo wamewakatalia wagombea wa Chadema katika maeneo hayo kuchukua fomu kwa kigezo kwamba ni siku moja ya Novemba 29 mwaka huu ndio ilikuwa imetengwa kwa ajili ya kuchukua fomu hizo.

“Kuna dosari katika maeneo ya Makuyuni, Mandaka huko tunashindwa kuelewa hawa wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ambao ni Maafisa Watendaji wanawazuia wagombea wetu kuchukua fomu kwa kigezo kuwa muda uliopaswa ni tarehe 29 mwezi wa kumi kitu ambacho tunaona ni ukiukwaji wa sheria za uchaguzi wa serikali za mitaa,” alisema Basil.

Lema aliongeza, “Hatujui wana maana gani wasimamizi hao, au hawakufunzwa namna ya kusimamia uchaguzi au ni harakati za kukisaidia Chama cha Mapinduzi (CCM).”

Kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu unaotarajiwa kufanyika Novemba 24 uchukuaji na urudishaji wa fomu za kugombea nafasi hizo na umeanza Oktoba 29 na utamalizika Novemba 4 mwaka huu.

0 Comments:

Post a Comment