Mkuu wa Wilaya ya Siha Onesmo Buswelu, amewaonya wanafunzi watakaothubutu kuchoma majengo, kuharibu miundombinu au kuiba mali za shule Serikali haitasita kuwachukulia hatua kali za kisheria.
Buswelu
alitoa kauli hiyo jana wakati wa hafla fupi ya kukabidhiwa mradi wa vyumba
vitatu vya madarasa yaliyojengwa katika shele ya Sekondari Sikirari iliyopo
kata ya Donyomurwaki na Serikali kupitia Wizara ya Elimu kupitia mradi wake wa
lipa kadiri ya matokeo makubwa sasa EP4R.
Alisema
wapo baadhi ya wanafunzi hususan wa shule za Sekondari, wamekuwa na mipango ya
kuchoma majengo ambayo yamejengwa kwa fedha nyingi, ambapo pia aliwataka
kujiepusha kuweka visasi na walimu wao kwani kwa kufanya hivyo kunasababisha
madhara ikiwemo kurudisha nyuma maendeleo ya shule.
DC Buswelu
alisema zipo baadhi ya shule nchini zimekuwa zikichomwa moto na baadhi ya
wanafunzi ambapo kwa upande mwingine inatokana na visasi visivyokuwa na tija
kwa maendeleo ya kielimu hivyo kuwataka wazazi na walezi kuwakanya watoto wao kutojihusisha na vurugu hizo.
“Serikali
ya Awamu ya Tano imefanya mambo makubwa sana katika wilaya ya Siha,
imeweza kutusaidia ujenzi wa madarasa,
mabweni katika sekta ya elimu kwenye shule za msingi na sekondari, lengo likiwa
ni kuzipatia ufumbuzi kero za walimu na wanafunzi,”alisema DC Buswelu.
Akizungumza
wakati wa makabidhiano hayo afisa Elimu sekondari wilaya ya Siha Mwl Herman Msasa alisema amefurahi kuona
ujenzi wa madarasa hayo ukimalizika kwa wakati na kuwataka wanafunzi kusoma kwa
bidii ili kuweza kufanikisha malengo yao ya kielimu.
"Kwanza
napenda nichukue fursa hii kuipongeza kamati ya ujenzi kwa kusimamia mradi huu
mpaka kukamilika kwake hizi ni jitihada kubwa sana kwanza kwa kumaliza ujenzi
huu ndani ya muda tuliokubaliana" alisema Mwl Msasa.
Aidha Mwl
Msasa aliwasihi wanafunzi kujitahidi kutunza mali za serikali yakiwemo
madarasa, madawati na samani nyingine ili ziweze kudumu kwa muda mrefu.
Kwa upande
wake Mkuu wa shule ya Sekondari ya Sikirari Mwl Kauka Akyoo, alisema shule hiyo ilipokea kiasi cha Sh milioni 60 kutoka Wizara ya Elimu kupitia mradi wake wa
lipa kadiri ya matokeo makubwa sasa (EP4R) kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vitatu
vya madarasa.
“Tunaishukuru
sana Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt.
Magufuli kwa kutoa elimu bila malipo pamoja na kutoa fedha za mradi
huu,”alisema Mwl Akyoo.
Aidha
alisema shule hiyo pia inakabiliwa na changamoto ya chumba kimoja cha darasa,
ofisi ya walimu, jengo la utawala, jiko,
bwalo la kulia chakula wanafunzi, bweni la wasichana pamoja na ukamilishwaji wa
maabara.
Imeandikwa na Kija Elias…..Oktoba 21, 2019
0 Comments:
Post a Comment