Monday, October 7, 2019

MAKTABA YA JAIZMELA: Vladimir Putin ni nani?


Oktoba 7, 1952 alizaliwa Rais wa sasa wa Russia Vladimir Putin. Putin alizaliwa Leningrad katika Urusi ya Kisovieti ambapo kwa sasa eneo hilo linafahamika kwa jina la Saint Petersburg. 

Alikuwa mtoto wa mwisho kati ya watu wa Vladimir Spiridonovich  Putin (1911-1999) na Maria Ivanovna Putina (1911-1998). 

Baba yake alikuwa mpishi wa Vladimir Lenin. Wakati anazaliwa Putin kaka zake wawili walikuwa wameshafariki dunia katikati ya miaka ya 1930. Kaka yake wa kwanza Albert alifariki akiwa mdogo na mwingine aliyefahamika kwa jina la Viktor alifariki kutokana na maradhi ya diphtheria ambayo hutokana na bacteria wanaoleta homa kali ikiwamo kuvimba koo. 

Mama yake Putin alikuwa mfanyakazi katika kiwanda  akitokea katika familia ya kijeshi ambayo baba yake alikuwa miongoni mwa wanajeshi wa vikosi vya majini vya Kisoviet mwanzoni mwa miaka ya 1930. 

Septemba 1, 1960 Putini alianza kusoma katika shule ya msingi No. 193 iliyokuwapo Baskov Lane karibu na nyumbani kwao. 

Putin alikuwa miongoni mwa wanafunzi akali ya 45 katika darasa alilokuwa akisoma ambao hawakuwa wanachama wa Jumuiya ya Lenin kwa vijana kati ya miaka 9-15 iliyofahamika kwa jina la Young Pioneers. 

Akiwa na umri wa miaka 12, alianza kujifunza sanaa za mapigano katika kategori ya sambo na judo. Aliwahi kutwaa mkanda mweusi kutoka katika Judo na pia Master wa mchezo wa Sambo. 

Putin alijifunza lugha ya Kijerumani alipokuwa katika elimu yake ya sekondari pale St. Petersburg 281 na hadi sasa anaongea vizuri lugha hiyo. 

Pia Putin alisoma masuala ya Sheria na kuhitimu katika Chuo Kikuu ya Leningrad ambacho kwa sasa kimebadilishwa jina na kuwa Chuo Kikuu cha St. Petersburg mwaka 1975.  

Putin aliwahi kuwa afisa usalama wa KGB kwa miaka 16 hadi alipopanda cheo na kuwa Luteni Kanali kabla hajajiuzulu mwaka 1991 ili kuingia katika siasa. 

Aliondoka St. Petersburg na kutua Moscow mwaka 1996 ambako aliungana na Rais wa wakati huo Boris Yeltsin akihudumu kama mkurugenzi wa idara ya usalama. 

Nafasi hiyo ilimpa kushika nafasi ya Waziri Mkuu na baadaye alishika madaraka ya Urais kwa muda baada ya Yeltsin alipojiuzulu Desemba 31, 1999. 

Katika kipindi chake cha kwanza cha Urais, uchumi wa taifa hilo ulikuwa imara kwa miaka yote minane. Machi 2018 alichaguliwa tena kushika wadhifa wa urais wa taifa hilo ambao utakoma 2024. 

Wachambuzi wa masuala ya siasa ulimwenguni wanasema katika kipindi cha Urais uwazi umeshuka ukienda sambamba na mapambano dhidi ya rushwa yamekuwa hafifu katika taifa hilo. 

Demokrasia imeshuka katika kipindi cha Putin. Maofisa wa Marekani wamekuwa wakimshutumu Putini kwa kuingilia uchaguzi mkuu wa 2016 uliomweka madarakani Donald Trump. 

Wawili hao ambao gazeti la Washington Post limewataja kuwa wamekuwa wakiwasiliana kwa siri zaidi ya mara 16 wamekuwa wakipinga tuhuma hizo. 

0 Comments:

Post a Comment