Chifu wa Kijadi wa Wilaya
ya Magonchi nchini Malawi maarufu kwa jina la Bwananyami amefariki dunia mapema
leo asubuhi katika hospitali ya Queen Elizabeth mjini Blantyre alikokuwa
amelazwa.
Chifu huyo wa Chowe ambaye jina lake halisi ni Atinga Sande alikuwa
maarufu nchini Malawi kwa harakati zake za kupigania elimu kwa wasichana.
Bwananyambi
alikuwa chifu wa vijiji 33 katika Chowe wilayani Mangochi.
Msemaji wa Serikali
za Mitaa na Maendeleo Vijijini Muhlabase Mughogho amethibitisha kutokea kwa
kifo cha chifu huyo aliyekuwa na ushawishi mkubwa.
Kwa mujibu wa mdogo wa
marehemu na mwenyekiti wa vijiji Balakasi amesema Bwananyambi alipelekwa katika
Hospitali ya Wilaya ya Mangochi wiki lililopita na aliruhusiwa siku tatu
zilizopita kabla ya hali yake kubadilika na kukimbizwa katika Hospitali ya
Queen Elizabeth siku ya Ijumaa.
Balakasi amesema dada yake alikuwa akilalamika
kuhusu shinikizo la damu. Taarifa ya Familia hiyo imesema Bwananyambi atazikwa
kesho katika makao makuu ya Wilaya ya Mangochi ya Ndumundu.
Mkuu wa wilaya ya
Mangochi Mchungaji Moses Chimphepo amemuelezea Bwananyambi, kuwa alikuwa
mpambanaji asiyechoka katika kuwapigania wasichana ili waweze kwenda shule.
Hivyo kuondoka kwake ni pengo kubwa katika wilaya na taifa la Malawi kwa
ujumla. Aidha Mkuu wa wilaya huyo amesema ni miongoni kati ya machifu waliokuwa
mbele katika kuzuia ndoa za utoto kwa wasichana ili waende shule kupata elimu.
Bwananyambi
alipambana kutunga sheria ndogo ndogo kwa ajili ya kuwaadhibu wazazi waliokuwa
wakiwaozesha kwa wanaume ambao walikuwa wakiwapeleka nchini Afrika Kusini.
Bwananyambi alichukua kiti cha Uchifu Juni 12, 1998. Miezi 12 iliyopita Bwananyambi
alinusuru ndoa 30 za watoto walio chini
ya umri wa miaka 18.
Asilimia 42 ya wasichana nchini Malawi huolewa kabla ya
kufikisha umri wa miaka 18. Mmoja kati ya kumi huolewa kabla ya kufikisha miaka
15 ambayo ni sawa na asilimia 9.
Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa
linaloshughulika na Watoto la UNICEF linasema Malawi ni nchi ya 12 ulimwenguni
kwa ndoa za utotoni.
UNICEF inasema wanawake wanaishi katika ukanda wa kati
huolewa wakiwa na umri mkubwa ukilinganisha na walioko katika mikoa ya
Kaskazini na Kusini mwa taifa hilo.
Takwimu za mwaka 2017 zinaonyesha endapo
taifa hilo litafanikiwa kuzuia ndoa za utotoni litajipatia kiasi cha dola
milioni 167 kwa mwaka.
Malawi imejifunga kuwa ifikapo 2030 itakuwa imefanikiwa kukabiliana
na changamoto hiyo ikiwa ni uwiano wa 5.3 ya Malengo ya Milenia (SDG’s).
0 Comments:
Post a Comment