Friday, July 3, 2020

MAKTABA YA JAIZMELA: Anna Maria Mozart ni nani?

Julai 3, 1778 alifariki dunia mama wa mwanamuziki kipaji kuwahi kutokea ulimwenguni Wolfgang Amadeus Mozart (1756-1791) Anna Maria Walburga Mozart.

Anna Maria pia alikuwa mama wa dada wa Wolfgang aliyefahamika kwa jina la Maria Anna Mozart (1751-1829). Anna Maria alizaliwa Desemba 25, 1720.

Alifariki dunia baada ya kupatwa na homa alipokuwa Paris huko nchini Ufaransa. Alizikwa katika makaburi ya Saint-Eustache.

Mnamo mwaka 1747 Anna liolewa na Leopold Mozart huko Salzburg. Mwandishi wa Historia kuhusu muziki raia wa Ujerumani Hermann Abert  aliwahi kuandika kwamba wawili hao enzi za maisha yao ya ndoa walionekana kuwa ni watanashi wa mjini Salzburg.

Baadaye waliondoka na kwenda kuishi katika mtaa ambao kwa sasa tangu mwaka 1996 umekuwa ni tunu ya kihistoria dunia wa Getreidegasse 9 nchini Austria kwani hapo katika ghorofa ya tatu alizaliwa Wolfgang Mozart.

Kuhamia katika mtaa huo kulitokana na urafiki mkubwa baina ya Mzee Mozart na kabaila mmoja aliyefahamika kwa jina la Lorenz Hagenauer ambaye alikuwa akisafiri nao mara kwa mara. 

Anna Maria alizaa watoto saba lakini wawili tu ndio waliofika ukubwa wengine wote waliaga dunia wakiwa bado wadogo.

Wakati anamzaa Wolfgang alinusurika kifo kutokana na kondo kusalia katika placenta. Watoto wawili waliobaki ndio waliistaajabisha dunia. 

Nannerl kama ambavyo walizoea kumwita alikuwa akisafiri na kaka yake katika kufanya matamasha ya muziki. Baadaye Wolfgang ndiye aliyekuwa wa pekee wa kwanza katika utunzi wa muziki duniani.

0 Comments:

Post a Comment