Tuesday, July 14, 2020

Wizara ya Fedha yashauriwa kuchapisha noti mpya ya Magufuli

Mkurugenzi  wa Taasisi ya Sanaa ya Kilimanjaro Cultural Heritage  Centre ya mkoani Kilimanjaro, Chifu Athuman Omari Mwariko, ameishauri Serikali kupitia Wizara ya fedha kutengeneza noti mpya za fedha na fedha hizo ziwekwe picha ya rais Dkt. Magufuli.

Hayo yanajiri ikiwa ni siku chache kupita baada ya Rais John Pombe Magufuli kupita kwa asilimia 100 katika kura za maoni za kuwania nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

Chifu Mwariko ambaye pia ni Kada wa CCM mkoani Kilimanjaro alisema amefurahishwa na utendaji kazi wa Rais Dkt. John Magufuli katika kipindi cha miaka mitano na kuweza kuifikisha nchi katika uchumi wa kati hivyo ameona anastahili kupewa heshima kwa kuchapishwa fedha mpya na picha yake kuwekwa kama nembo ya taifa kwa heshima ya aina yake.

“Itakuwa kumbukumbu nzuri endapo Magufuli atawekwa kwenye noti ya Shilingi 50,000 ambayo inasadifu maendeleo makubwa ya uchumi wa kati wa viwanda ambao ameufikia kabla ya muda wa malengo yake ya 2025, hilo ni jambo la kupongeza lakini lisifanywe kwa maneno pekee liwekwe kwenye vitu kama fedha yetu,” alisema Mwariko.

Aidha Chifu Mwariko alisema kupewa asilimia 100 ni kuonyesha nia ya dhati na utendaji wake uliotukuka kwa ardhi ya Tanzania na viunga vyake kwani kwa muda mrefu kumekuwa na mateso makubwa katika suala la uchumi.

Alisema Tanzania imeingia katika uchumi wa kati wa mujibu wa takwimu za Benki ya Dunia  katika mwaka mpya wa fedha ambao ulianza tangu Julai mosi hivyo kujiunga na mataifa saba ya eneo la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara. Kwa mujibu wa dira yake ya maendeleo Tanzania ilipanga kuingia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

“Naishauri Serikali  kutengeneza noti mpya za fedha na kuchapisha picha ya Dkt. Magufuli, kwa sababu ameonyesha mambo makubwa ikiwemo kufanikisha kufikia uchumi wa kati,”alisema Mwariko.

Aidha Mwariko alisema Rais Dkt. Magufuli amefanikiwa kwa kuweka rekodi nzuri katika kupanua na kuboresha miundombinu kama  vile barabara, umeme na kufanya mabadiliko makubwa katika sekta ya madini.

''Yapo mabadiliko makubwa  ndani ya serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais magufuli, mafanikio hayo ni pamoja na kuzuia utoroshaji wa madini kwenda nje ya nchi kwa kufungua masoko ya madini katika kila mkoa, ili kuongeza ushirikishwaji wachimbaji wadogo,'' alisema.

Tangu Januari 2011 Benki Kuu ya Tanzania iliongeza noti mpya za shilingi 500, 1000, 2000, 5000 na 10,000 huku Wizara ya Fedha na Uchumi inasimamia mapato, matumizi na kuigharimia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jumla na kuishauri Serikali katika mambo mengi ya fedha kusaidia malengo ya kijamii na kiuchumi ya Serikali. 



0 Comments:

Post a Comment