James Monroe alizaliwa Aprili 28, 1758 huko
Westmoreland, Virginia na akafariki dunia Julai 4, 1831 jijini New York. Alifariki
dunia akiwa na umri wa miaka 73 ukiwa ni mwaka mmoja baada ya mkewe kufariki
dunia. Monroe alizikwa katika makaburi ya Hollywood huko Oregon Hill, Virginia.
Monroe ni miongoni mwa marais watatu waliofariki Julai
4 kwa miaka tofauti walioliongoza taifa la Marekani. Wengine ni Thomas Jefferson
na John Adams. Pia watatu hawa ndio waanzilishi wa taifa la Marekani. Monroe alikuwa Rais wa tano wa Marekani.
Aliliongoza taifa hilo kutoka mwaka 1817 hadi 1825.
Monroe anakumbukwa kutokana na umuhimu kwa Marekani hususani sera za kigeni za
taifa hilo.
Mpaka sasa Maandiko ya Monroe ndio yanayoongoza taifa
hilo katika sera za nje ambapo aliyaonya mataifa ya Ulaya kuingilia masuala ya
Magharibi. Kipindi alichokuwa akiongoza taifa hilo kilikuwa kikifahamika kama ‘Zama
za Hisia Nzuri’ (Era of Good Feelings).
Wananchi wa Marekani walikiita hivyo huenda kutokana
na namna Utawala wa James Madison ulifanya kisha namna Monroe alivyoweza
kusuluhisha baadhi ya mambo ambayo yalikuwa yakienda mrama wakati wa Madison.
Pia vyanzo vingine vinasema kauli hiyo ilianza
kutumika kuanzia mwaka 1815 baada ya kuisha kwa vita vya Napoleoni, kwani raia
wa Marekani walianza kuishi kwa raha na kutoyaangalia mataifa ya Ulaya katika
masuala ya kisiasa na kijeshi. Monroe alipitisha msimamo huo wa sera za kigeni
za taifa hilo mnamo Desemba 2, 1823 wakati akilihutubia Bunge la Kongresi.
Monroe alitangaza kwamba Dunia ya zamani na Dunia Mpya
zina mifumo tofauti na zinatakiwa zisalie kuwa tofauti. Monroe alichanganua
kauli hiyo katika maeneo manne.
1. Marekani haitaingilia masuala ya ndani au vita vya
mataifa ya Ulaya.
2. Marekani inayatambua na kwamba haitaingilia
makoloni yaliyokuwapo na utegemezi wao katika ardhi hiyo.
3. Upande wa Magharibi utasalia kwa ajili ya ukoloni
ujao. 4. Jaribio lolote ambalo litafanywa na taifa lolote kutoka Ulaya kwa
ajili ya kutaka kushikilia eneo lolote katika bara la Amerika litachukuliwa
kama ni kitendo cha uhasama dhidi ya Marekani. Monroe aliingia madarakani akiwa
katika muungano wa vyama vya Democratic-Republican ulioasisiwa na Jefferson.
Monroe alizaliwa kwa baba kutoka Uskochi aliyefahamika
kwa jina la Spence Monroe na mama kutoka Wales Elizabeth Jones. Familia yao
ilikuwa ya kikabaila ambayo ilimiliki kiasi cha ekari 600 huko Virginia.
Akiwa na umri wa miaka 16 aliingia katika chuo cha
William & Mary lakini mwaka 1776 aliondoka kwa ajili ya kwenda vitani
kupigana kwa ajili ya Mapinduzi ya Marekani.
Akiwa Luteni alipita katika maeneo ya Delaware akiwa
na Jenerali George Washington katika vita ya
Trenton. Katika vita hiyo Monroe aliumia bega vibaya sana, hivyo
akaondolewa katika uwanja wa vita. Baada ya kupona alirudi na kupandishwa cheo
kwa ushujaa wake katika vita akawa Captain.
Akiwa katika cho kipya alipigana katika vita vya
Brandywine na Germantown. Alipanda tena katika cheo na kuwa Meja na akawa
msaidizi wa Jenerali William Alexander aliyefahamika sana kwa jina la Lord
Stirling.
Akiwa na Lord Stirling walipambana katika hali ya
taabu sana wakiwa na majeshi kwenye bonde la Forge wakati wa majira ya baridi
mnamo mwaka 1777-1778. Pia Monroe alikuwa skauti wa Washington wakati wa vita
vya Monmouth na wakati huo huo alikuwa akimsaidia Jenerali Lord Stirling katika
masuala ya utawala wa kijeshi.
Mnamo mwaka 1780 Monroe alijiuzulu kufanya kazi na
jeshi na alianza kusoma masomo ya Sheria
akiwa mikononi mwa Thomas Jefferson ambaye wakati huo alikuwa gavana wa
Virginia na wawili hao walitengeneza muungano ambao ulikuwa wa kweli na imara.
0 Comments:
Post a Comment