Wednesday, July 8, 2020

MAKTABA YA JAIZMELA: Kim Il-sung ni nani?

Julai 8, 1994 alifariki dunia mwanzilishi wa taifa la Korea ya Kaskazini Kim Il-Sung. Alizaliwa huko Kim Song-ju mnamo Aprili 15, 1912. Alilitawala taifa hilo tangu kuanzishwa kwake mwaka 1948 hadi mauti yake.

Alikuwa Waziri Mkuu kutoka mwaka 1948 hadi 1972 na baadaye akawa Rais kutoka mwaka 1972 hadi kifo chake. Il Sung alikuwa kiongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Korea (WPK) kutoka mwaka 1949 hadi kifo chake.

Miaka ya mwanzoni ya kuanzishwa kwa taifa hilo alikuwa akifahamika kama Mwenyekiti wa chama hicho hadi 1966. Baada ya hapo alianza kutumia cheo cha Katibu Mkuu wa Chama.

Aliingia madarakani baada ya utawala wa Japan kuondoka nchini mnamo mwaka 1945. Il Sung aliidhinisha uvamizi wa Korea Kusini mnamo mwaka 1950, upinzani mkali wa kijeshi Korea Kusini uliokuwa ukifadhiliwa na  Umoja wa Mataifa  ukiongozwa na Marekani.

Kutulia kwa sakati hilo kulifanywa mnamo Julai 27, 1953 baada ya kuingia makubaliano. Il Sung anakuwa mtawala wa tatu kukalia kiti cha urais  kwa muda mrefu katika karne ya 20 akikaa madarakani kwa miaka 45.

Katika utawala wake licha ya kwamba Il Sung alikuwa hakubaliani na sera za Stalin wa Urusi wakati huo lakini haikuwa rasmi kwamba alikuwa na uhusiano wa karibu na Muungano huo wa Kisovieti.

Pia Il Sung hakushiriki mkutano wa kujitenga baina ya China na Urusi katika kipindi cha kutoka mwaka 1956–1966. Baada ya kuondoka kwa Khrushchev madarakani na nafasi yale kuchukuliwa na Leonid Brezhnev mnamo mwaka 1964 uhusiano wa Il Sung na Muungano wa Kisovieti ulikuwa mkubwa.

Il Sung alifariki dunia baada ya shambulio la ghafla la moyo akiwa katika makazi yake huko Hyangsan, kaskazini mwa Pyongyan. Baada ya shambulio hilo Kim Jong-Il aliamuru timu ya madaktari waliokuwa karibu na baba yake kuondoka na akapanga madaktari wengine bora zaidi katika safu hiyo.

Baada ya saa chache madaktari kutoka Pyongyan waliwasili licha ya jitihada za kuokoa uhai wake lakini ilishindikana na siku iliyofuata alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 82.

Ibada ya kimila ya Wakofyushan (Confucians) ilifanyika na kifo chake kilitangazwa rasmi saa 30 baadaye.

Kifo cha Il Sung kiliombolezwa nchini humo kwa siku 10 na akatangazwa mtoto wake Kim Jong-Il kukalia mahali pake. Julai 17, 1994 Pyongyan ilishuhudiwa mamia ya watu wakihudhuria mazishi ya kiongozi huyo.

Mwili wake uliwekwa katika hadhira huko Kumsusan katika Jumba la Jua ambako alilazwa katika jeneza la kioo ili watu wote waweze kumwona na kutoa heshima zao za mwisho.

Bendera ya Chama cha Wafanyakazi alichokuwa akikiongoza ilifunikwa katika mwili wake. Enzi za uhai wake Il Sung aliandika kazi nyingi.

Vyanzo nchini Korea kaskazini vinasema hotuba zinakadiriwa kufikia 10,800, ripoti, vitabu, mikataba n.k  zimehifadhiwa.

Chache kati ya hizo zimewekwa kwenye kazi za Kim Il Sung (김일성전집). Muda mchache kabla ya kifo chake Il Sung alichapisha kitabu cha historia yake katika matoleo manane kinachofahamika kwa jina la ‘With the Century’. 

0 Comments:

Post a Comment