DAR ES SALAAM, TANZANIA
Makala yaliyopita tulijikita
kuangazia maisha ya awali ya mwanariadha na mwanamapinduzi katika mchezo huo
Ron William Davis na namna alivyopata nafasi ya kuzuru bara la Afrika.
Aidha katika tuliangazia
namna alivyokutana na mpiganaji wa taifa la Afrika Kusini Nelson Mandela
mwanzoni mwa miaka ya 1990 ambaye alitumia mchezo wa riadha kuomba radhi wanamichezo
wa Afrika Kusini ambao walifungiwa kushiriki michuano tangu mwaka 1960 kutokana
na vitendo vya ubaguzi wa rangi.
Tuliona Mandela alipopaza
sauti yake kwa watu wa Afrika ya Kusini walimwelewa na ikawa sababu mojawapo
iliyomfanya akalie kiti cha urais wa taifa hilo mwaka 1994 ikiwa ni miaka
michache baada ya kutoka jela la Rhode Island alikodumu kwa miaka 27.
Katika makala haya
tutaangazia namna alivyotua Tanzania na kuwa kocha mkuu wa timu ya riadha ya
taifa. Kwa ufupi Ron Davis ndiye kocha wa kwanza kuiletea Tanzania medali pale
alipomsimamia mkongwe Filbert Bayi na Suleiman Nyambui katika mashindano ya
kimataifa.
MICHUANO YA JUMUIYA YA
MADOLA 1978
Mwaka 1978 michuano ya
Jumuiya ya Madola ilifanyika mjini Edmonton, Alberta nchini Canada. Nigeria
iliamua kuwa haitashiriki michuano hiyo kwani ilikuwa imetoka kwenye michuano
ya All Africa Games ambayo Ron Davis alikuwa kocha huko.
Sababu kubwa ya Nigeria ya
kutoshiriki ilikuwa wazi kabisa kwa ilikuwa imegomea kuunga mkono michuano hiyo
kutokana na New Zealand kushiriki mashindano ya michezo na taifa la Afrika
Kusini wakati huo ubaguzi wa rangi ulikuwa wa kiwango cha juu.
Kitendo hicho cha Nigeria
kufanya hivyo hakikuwa kigeni kwani mwaka 1972 iliongoza mgomo wa michuano ya
Olimpiki ilifanyika mjini Munich nchini Ujerumani pia ilifanya hivyo katika
Michuano ya Olimpiki ya mwaka 1976 iliyofanyika Montreal nchini Canada.
Katika mahojiano na Ron
Davis anasema, “Nigeria ilikuwa na msimamo wa kuunga mkono mapambano dhidi ya
ubaguzi wa rangi ambao ulikuwa ukienea kwa kasi, na juhudi hizo zilienea
duniano kote.” Ron Davis analikumbuka vema tukio hilo la michuano ya Jumuiya ya
Madola kwani taifa la Canada ambao walikuwa wenyeji wa mashindano hayo
walipeleka ndege yao Air Canada nchini Algeria ambayo ilitumika kuchukua
wanamichezo wa Afrika ambao walikwenda kushiriki.
Kocha huyo anasema, “Mimi,
Lee Evans na John Carlos hatukupanda ndege hiyo na timu lakini tulitumia ndege
ya Ujerumani kwa ufadhili wa kampuni ya Puma, kwani Carlos alikuwa
akiiwakilisha Puma katika michuano ya Jumuiya ya Madola.”
Ron Davis anasema kuwa uwepo
wa Carlos uliwafaidisha kwani baada ya siku kadhaa za kuwapo mjini
Herzogenaurach miongoni mwa vitongoji mahiri katika jimbo la Bavaria nchini
Ujerumani yeye na Carlos walikwenda Edmonton wakati Lee aliitwa California.
Akiwa kwenye ndege Ron Davis
anasema alikuwa haamini kama anakwenda kwenye michuano hiyo akiwa kama kocha na
alitabasamu tu akikumbuka miaka ya nyuma ilivyokuwa katika kufikia ndoto zake.
Canada haikuwa mara yake ya kwanza lakini safari ya kutinga katika michuano
hiyo kama miongoni mwa makocha wakubwa duniani ndiyo ilimfanya atabasamu ndani
ya ndege.
Wakati naandika makala haya
nikakumbuka nukuu ya mwanamitindo na mwigizaji wa kike wa Marekani Christie
Brinkley aliposema, “Ishirikishe dunia na tabasamu lako. Ni alama ya mahusiano
mazuri (urafiki) na amani.”
Hakika hata sasa ukimuona
Ron Davis tabasamu lake bado analo hiyo ikimaanisha ndiye yule aliyetabasamu
ndani ya ndege ikimaanisha ni mtu wa amani. Na amani yake ndiyo ilimfanye
akutane na ujumbe kutoka Tanzania katika michuano hiyo.
HATUA MOJA MBELE
Ron Davis akihojiwa na mwandishi wa habari Jabir Johnson Novemba 2018 Mkuza, Kibaha mkoani Pwani. |
Aidha Ron Davis alikuwa
hajui kwa wakati huo alipokutana na kocha wa Filbert Bayi kama ingetengeneza
njia. Wakati huo kocha Sulus alikuwa akimnoa Bayi. Baada ya mazungumzo ya muda
Sulus alimtambuliza kwa Waziri wa Michezo na Utamaduni wa Tanzania alikuwapo
Edmonton.
Hapo ndipo walipopanga muda
mzuri wa kukutana ili kubadilishana mawazo na uzoefu kuhusu mchezo wa riadha.
Ron Davis anasema alishtushwa na namna mwakilishi huyo wa nchi alivyomkaribisha
kutokana na kwamba alikuwa bado ni kocha wa timu ya taifa ya Nigeria ingeleta
mkanganyiko lakini alisubiri nini kitakachotokea.
Unafikiri nini kilifuata
baada ya Ron Davis kukutana Kocha Sulus na Waziri wa Michezo na Utamaduni
katika mashindano ya Jumuiya ya Madola mwaka 1978? Tukutane juma lijalo katika
mwendelezo wa makala haya.
Makala haya yametayarishwa
na Jabir Johnson ambaye alipata fursa ya kuzungumza na Ron Davis katika
masuala mbalimbali ya maisha yake na medani ya riadha alipotua nchini Tanzania. Pia yalichapishwa katika Gazeti la Tanzania Daima. Kwa maoni ushauri barua pepe: jaizmela2010@gmail.com
0 Comments:
Post a Comment