Tuesday, May 19, 2020

"Mo Dewji apewe asilimia 51"

Wanachama wa klabu ya Simba nchini wametakiwa kuchukua maamuzi magumu dhidi ya mwekezaji wao Mo Dewji kwa kumpa asilimia 51 ya umiliki wa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Akizungumza katika mahojiano maalum na gazeti hili mfanyabiashara maarufu mjini Moshi mkoani Kilimanjaro James Serengia alisema mwenendo ilionao kwa sasa klabu hiyo hauridhishi licha ya kuwa na wachezaji wazuri wa kiwango cha kimataifa.

“Kinachomkwamisha Mo, ni wanachama wa Simba wenyewe wampe asilimia 51 za hisa ili iendane na soka la kisasa wewe huoni vilabu vikubwa barani Ulaya vinavyofanya, dunia ipo katika mfumo wa ubepari inabidi hata Simba wawe hivyo mapema kama wanataka mafanikio makubwa,” alisema Serengia.

Aidha mfanyabiashara huyo alisisitiza kuwa kwa sasa hali ya uwekezaji katika klabu hiyo sio mbaya sana lakini bado haitoshelezi soka la kisasa kwani kuwa na asilimia 49 kutasababisha kila kukicha kujikita katika hoja nyepesi zisizo na mashiko.

Katika suala la kutafuta vipaji vya wachezaji mdau huyo wa soka nchini alisema kumekuwa na urasimu kwani wachezaji wanaoletwa hawakidhi viwango na wengine umri wao unawatupa mkono.

“Unapomzungumzia Okwi kurudi Simba, unazungumzia umri wake je utaweza kuendana na mahitaji ya sasa, Kagere mwenyewe umri huo unamtupa mkono, Pascal Wawa naye miaka ndio hiyo, sasa hapo nafirikiri maslahi binafsi au maslahi kwa wachache ndio yatakayoimaliza Simba, dawa ni kumpa Mo umiliki kamili,” alisema Serengia.

Serengia alisisitiza kuwa mipango ya ndani ya Simba katika kutafuta vipaji vya wachezaji ni kwamba wanapaswa kufikiria kuwekeza kwa vijana wenye umri mdogo akitolea mfano timu ya taifa ya Eritrea iliyocheza michuano iliyopita ya Cecafa.

“Utakumbuka wakati Eritrea ikicheza katika Cecafa wale vijana wako fiti sana tu, lakini mazingira yao sio mazuri sasa ukiwapata kutoka mle wanne tu kisha ukawapeleka Simba, wanakuwa hatari kuliko maelezo, kwanza kwao hali ni ngumu ya kimaisha kwa fedha ya Simba pale hakika hawagomi,” aliongeza Serengia.

Serengia alisema watani zao wa jadi Yanga wanaonekana kuamka na kutaka ufalme uendelee kusalia jangwani kutokana na mipango waliyonayo kwa sasa hivyo Simba kwa ilipofikia haipaswi kuonekana kuwa ni klabu ya kawaida.

0 Comments:

Post a Comment