Sunday, May 3, 2020

Wanawake wajawazito Mwanga waenda na ndoo za maji kujifungua


Wanawake wajawazito wilaya Mwanga, Mkoani Kilimanjaro wanalazimika kwenda na ndoo za maji pindi wakati wao wa kujifungua unapofika.

Hayo yalijiri katika  Mkutano wa Baraza la Halmashauri ya Wilaya hiyo wakati wa uwasilishwaji wa taarifa za robo ya tatu ya mwaka ya Januari hadi Machi katika mwaka wa fedha 2019/2020.

Akizungumza na gazeti hili Diwani wa Kata ya Kwakoa wilayani humo Dkt. Rogers Msangi alisema zahanati iliyopo katika kata yake wanalazimika kwenda na ndoo za maji.

“Akina Mama wajawazito wanawajibika kwenda nan doo za maji kujifungua katika zahanati ile, wanapokwenda kujifungua wanaambiwa waende na ndoo za maji, kwa sasa wamama wajawazito wanalazimika kujifungulia majumbani,” alisema Dkt. Rogers.

Dkt. Rogers aliweka sababu zinazosababisha kwa wanawake hao kwenda na ndoo za maji wakati wa kujifungua huku akisisitiza kuwa kilio hicho ni cha muda mrefu.

“Zahanati ya Kwakoa miundombinu yake ni mibovu, kilio hiki nimekiwasilisha kwa muda mrefu tangu Mwaka 2016 hakuna hatua iliyokwisha kuchukuliwa hadi sasa,” alisema Dkt. Rogers.

Hata hivyo Dkt. Rogers aliitaka halmashauri ya wilaya ya Mwanga kutupia macho zahanati hiyo kwa kuwa wakazi wa kata yake na kata za jirani imekuwa mkombozi kwao.

“Naiomba Halmashauri na Serikali Kuu iweze kuitupia macho Zahanati ile ili wananchi waweze kupata huduma stahiki kama ilivyo kwa wengine,” aliongeza Dkt. Rogers.

Mbali na hilo Mwenyekiti wa Kamati ya  Elimu Afya na Maji  ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kigonigoni Jeremiah Shayo aliweka bayana kuhusu mapambano dhidi ya maambukizi ya Corona kuwa bado inahitajika jitahada zaidi.

“Wataalamu wa afya kwenye maeneo ya vijijini hawana vifaa vya kujikinga na maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa Corona, jana mimi nilienda katika kituo cha Afya Kisangara kwa ajili ya kupima afya yangu lakini hata wale watoa huduma ambao niliwakuta wanatoa huduma hiyo walikuwa hawana vifaa vya kujinga hali ambayo inahatarisha usalama wao,” alisema Shayo.

Kwa upande wake Enea Mrutu Diwani Kata ya Shingatini alisema kwa sasa watu wa maeneo ya vijijini wanaogopa kwenda hospitalini kupima Malaria kwa kuhofia kuwekwa siku 14.

“Kwa sasa shivi madaktari wanapokukuta na joto kali wanawaweka karantini hali ambayo imekuwa ni hofu kubwa kwa wananchi kwenda hospitalini,” alisema Mrutu.

Hata hivyo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mwanga Teresia Msangi aliwataka wananchi kujihadhari sana na ugonjwa wa Covid 19 kwa kuchukua tahadhari, kwenye kata zetu kwa kuwaelimisha wananchi, wafahamu janga hili, na yale yote yanayoelekezwa na wataalamu wa afya, kujikinga na janga hili la Corona


0 Comments:

Post a Comment