Kaya 13 katika kijiji cha Gundusine wilayani Same mkoani Kilimanjaro zipo katika sintofahamu kuhusu ekari 106 za ardhi baada ya hukumu ya mahakama ya baraza la Ardhi na Nyumba kuamuru kurudishwa kwa ekari hizo kwa familia za wanakijiji hao kupuuzwa.
Hayo yanajiri baada mgogoro wa muda mrefu wa ekari 106 zilizopo katika kitongoji cha Gundu kijijini hapo kwa kile kinachoelezwa ni kuingilia eneo la mamlaka ya hifadhi.
Katika hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Baraza la Ardhi na Nyumba wilaya ya Same mkoani hapa Shauri Na. 29 la mwaka 2019 ilidaiwa kuwa Januari 30 mwaka huu mahakama ya baraza hili liliamuru mdaiwa ambaye ni Baraza la Kijiji cha Gundusine pamoja na wakala wake au mtu yeyote aliyeshikilia ardhi au kulima mazao ya eneo hilo waache kulitumia na kuwakabidhi Wadai ambao ni Yohana Mkondo na wenzake.
Dalali wa Mahakama Baraza la Ardhi na Nyumba wilayani humo Msuya Auction Mart ilipewa idhini ya ya kwenda kuhakikisha wadai wanapewa eneo hilo kwa mujibu wa hukumu iliyotolewa hapo Januari 30 mwaka huu.
Mnamo Machi 11 mwaka huu Msuya Auction Mart ilifika katika eneo la kijiji cha Gundusine, kilichopo katika kata ya Hedaru na kumfukuza mdaiwa na wakala wake kisha kuwa kuwakabidhi wadai eneo la shamba likiwa na mazao na miti katika utekelezaji uliofanyika kwa amani na utulivu mbele ya mashahidi baada ya taarifa kutolewa na uongozi wa kijiji na ngazi nyingine.
Wadai wa shamba hilo ambao ni wakulima wa Ngurunga waliokabidhiwa kwa idhini ya mahakama Machi 11, mwaka huu ni Elinazi Nisagurwe, Elifadhi Amani, Yohana Nkondo, Mbonea Abrahamu, Joeli Nisagurwe, Saimoni Samiseli, Anderson Eneza, Abrahamu Elisamehe, Yona Nkondo, Musa Mbonea Yonadha Nisagurwe
Ekari 106 za mashamba zimepandwa mazao kama maparachichi, miembe, mifenesi, mistafeli, mayungwa (maombo) na miti.
Aidha uamuzi huo ulisema Nkondo na wenzake na wakala wanayohaki ya kutumia ardhi hiyo kwa kulima au kuendeleza bila kubughudhiwa na yeyote atakayeingia katika shamba hilo kwa nia ya kufanya fujo au kuharibu mali au mipaka wachukuliwe hatua za kisheria.
Hata hivyo baada ya hayo wadai hao wamepatwa na sintofahamu, wanasema tangu walipopewa wamejikuta mikononi mwa polisi kwasababu ya kuonekana wakilima katika eneo la hifadhi huku wakiitaja ofisi ya kata ya Hedaru kuhusu na mgogoro huo.
“Tunasikitika eneo letu linadaiwa kuwa lipo ndani ya hifadhi wakati mahakama iliamua kuwa hili ni eneo letu, wanatuletea askari eti kwasababu tumelima eneo la hifadhi wakati sisi tumelima mashamba yetu tuliyokabidhiwa na mahakama kisheria, tumewekwa lokapu bila sababu,” alisema Saimon Kiondo mmojawapo wa wadai wa ardhi hiyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Gundusine Tumsifu Ngoyo alikiri kuwa na mgogoro huo na kwamba kilichofanywa na mahakama hakikubaliki kwani wadai walivamia hifadhi hiyo na alama za hifadhi zinaonekana ndani ya mashamba hayo ya Ngurunga.
“Hata juzi wamekuja watu kutoka taifa na askari mpelelezi ili kujiridhisha na uamuzi wa mahakama, bikoni zinazonyesha wamevamia eneo la hifadhi halafu pia suala hili linafahamika sana katika ofisi ya mtendaji wa kata ya Hedaru,” alisema Ngoyo.
Mgogoro huo wa ardhi ni wa muda mrefu kutoka miaka ya 1994 mpaka hivi sasa bado unazidisha sintofahamu miongoni wa wanakijiji wa Gundusine.
0 Comments:
Post a Comment