Omary Mwariko |
Msanii wa kitaifa na
kimataifa Omary Mwariko amependekeza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo imefanyiwe marekebisho mapya ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa
majukumu yake.
Akizungumza na
gazeti hili msanii huyo ambaye ndiye aliyechonga kifimbo cha Baba wa Taifa
Mwalimu Julius Nyerere alisema miongoni mwa marekebisho yanayotakiwa kufanyika
ni kuondoa utamaduni ambao ingefaa utengenezewe wizara yake.
“Lugha zetu, muziki
wetu, ngoma zetu, historia, matambiko yetu, falsafa na dini zetu za asili
zingepata kuangaliwa kwa kina, kinachofanyika sasa ni maneno tu ambayo hayawezi
kututoa hapa tulipo ingefaa utamaduni utengenezewe wizara yake,” alisema
Mwariko.
Mwariko alisema
mpaka sana kipengele cha utamaduni hakijapewa nafasi ya kutosha katika wizara
hiyo na ndio sababu kimekuwa kama mtoto yatima ndani ya Wizara hiyo.
“Viongozi wa kijadi
kama wazee wa kaya, wazee wa ukoo na watemi pamoja na mila za jadi, desturi na
siasa za asili katika mila za Kitanzania hazijapewa uwanja mkubwa katika wizara
kinachoonekana ni masuala ya sanaa kwa kiasi kidogo na michezo kwa kiasi
kikubwa,” aliongeza.
Aidha msanii huyo
aliongeza utamaduni ukitengewa wizara yake katika uteuzi wa watendaji ni vema
wakaangaliwa wale ambao wamekubuhu katika utamaduni badala ya kujali vyeo vya
kisiasa ambavyo wakati mwingine vinakosa afya ya kutekeleza majukumu yake
kutokana na waziri husika kukosa uelewa wa kutosha wa masuala hayo.
“Itasaidia sana
kumpata waziri wa utamaduni ambaye anayajua vizuri masuala ya utamaduni kwa
kina kwa kufanya hivyo atakuwa ameitendea haki wizara husika,” alisema.
Mwariko alisema
wachoraji, wachongaji, waganga wa kienyeji, wachawi na walogaji hawajapewa
nafasi ya kutosha wafanye yao na kuongeza kwamba ustaarabu wa Kimagharibi
umeharibu kabisa ladha halisi ya mila na desturi za Kitanzania.
“Ukimwambia mtu
mlogaji ni mtu muhimu atakwambia Mungu amekataza kumloga mtu, sasa kumbe
ustaarabu wa Kimagharibi ulipofika ulishusha yetu ili kupandisha yao sasa mbinu
iliyotumika ni kwa kutumia dini, lakini kuna ulazima wa kurudisha mila na
desturi zetu la sivyo zitapotea hivi hivi,” alisema Mwariko.
Mwariko akizungumza jambo mbele ya mwandishi wa habari Jabir Johnson Mei 12, 2020 mjini Moshi. |
0 Comments:
Post a Comment