Katika jamii yoyote mtu mwenye tabia ya umbea huchukiwa,
hutengwa na hata wakati mwingine hupigwa kwa kuonekana kuwa ni chanzo cha
migogoro na huku viongozi wa dini wakimwona mtu wa aina hiyo kuwa ni mtenda
dhambi.
Kuna waandishi wa vitabu mbalimbali wanatetea suala la
umbea kama Mwanasaikolojia wa Russia na mwandishi wa kitabu kiitwacho ‘Nguvu ya
Umbea’, Maria Konnikova anasema hakuna mtu anayeweza kuukwepa umbea na kushauri
kuwa mtu asihangaike kutaka kuwazuia wambea kusema wayatakayo.
Ninafahamu kuwa katika maisha ya uandishi wa habari kuna
mahali tunakosea kama zilivyo kada nyingine za udaktari, ualimu na kadhalika
kwani hakuna hata mmoja ambaye amekamilika asilimia zote.
Nakubaliana na baadhi ya makosa yanayofanyika na
waandishi wachache ambao nafikiri neno hili ‘umbea’ limekuwa likitumika
kuwakilisha waandishi wa habari. Utasikia mitaani baadhi ya maneno”…huyo
mwandishi wa habari anakuja…” wakimaanisha mmbea anakuja.
Tafsiri mbalimbali za neno umbea zinaonyesha kuwa ni
mazungumzo ya ovyo ovyo yasiyo ya maana. Ninafahamu kuwa asili ya mwanadamu ni
kuzungumza japokuwa wakati mwingine hujikuta akiishia kutoa mifano halisi ya
maisha ya watu wengine na hivyo kuingia katika mgogoro wakati mtu aliyesemwa
anaposikia.
Ningependa kila mtanzania afahamu kuwa kuwaita waandishi
wa habari wambea sio jambo la heshima na la kiuungwana. Waandishi wa habari
tumekuwa mbele kuuhabarisha umma kwa kadri tunavyoweza katika hali ngumu na furaha
lakini hatimaye shukrani ya punda ni mateke mnatuita majina yasiyofaa.
Imefikia hatua mkikaa vijiweni mnasema kwa sasa uandishi
wa habari hakuna, stori zao ni nyepesi zisizo na mashiko, hazigusi wananchi
halafu wakati huohuo mkiona mmebanwa mnaanza kutuita waandishi wa habari wakati
mwingine tunaambulia matusi kwa mmoja mmoja au kama tasnia kwamba hatujikiti
kufuatilia kwa kina; hivi kweli moyo huo tunaupata wapi wakati mnatuita majina
ya kukera kama sisi wambea? Sisi ni binadamu tunastahili heshima kama binadamu
wengine, Kama ni umbea kaeni nao ninyi wenyewe.
Hii ni taaluma yenye misingi yake sasa kutuita wambea ni
kutukosea heshima na si jambo la kiuungwana. Utu ambao huzaa ushirikiano na
mshikamano ukikosekana baina yetu na ninyi wananchi itakuwa ni vurugu.
Kwani neno letu moja linaweza kuwasha msitu. Tumeshuhudia
baadhi ya nchi kalamu na karatasi ya mwandishi wa habari ilipotumika vibaya
ilileta maafa katika eneo husika amani ilivurugika kabisa. Hatupendi tufike
huko tunataka Tanzania yenye utashi.
Ningewaomba watanzania ondoeni maneno ya kejeli katika fani hii ili
tuijenge Tanzania yetu.
0 Comments:
Post a Comment