Wanawake nchini wametakiwa kujiendeleza kielimu ili kuongeza nafasi ya kuwania uongozi katika kada mbalimbali hatua ambayo itakuwa mwendelezo wa juhudi za wanaharakati mbalimbali za kutaka usawa na kuwa chachu ya mawendeleo.
Akizungumza katika mahojiano maalum aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi Mjini Bi. Bernadetha Kinabo alisema mojawapo ya kikwazo za wanawake kupata uongozi wa kufanya maamuzi katika jamii ni elimu huku akisisitiza ulazima wa wanawake kuachana na dhana kuwa watabebwa tu.
“Nchi za Scandinavia wapo wanawake ambao ni Marais na Mawaziri wakuu wanatawala hadi leo, hao waote ni wasomi, wana elimu zao. Hapa Tanzania Baba wa Taifa hayati Mwalimu Nyerere aliweka misingi mizuri kwa akina Mama alishirikiana nao bega kwa bega katika utawala wake,unamkumbuka Lucy Lameck, Bibi Titi,” alisema Bi. Kinabo.
Bi. Kinabo aliwataka wanawake wasikwamishwe na vikwazo vinavyojitokeza mbele yao bali wajitahidi kupambana navyo ili kufikia malengo hasa ikizingatiwa mwaka huu ni wa uchaguzi
“Ukiangalia katika Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania asilimia 36 ni wanawake, Bunge la Rwanda asilimia 48 wanawake, ningependa kuwaona akinamama wenzangu kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi, katika manispaa ya Moshi takwimu zinaonyesha, idadi ya watu zaidi ya asilimia 51 ni wanawake hivyo huwezi kuwadharau katika kuleta maendeleo,” alisema Bi. Kinabo.
Hata hivyo alitoa wito wa wanawake kujituma pindi wanapopata nafasi za uongozi katika kada mbalimbali ikiwamo siasa na kutakiwa kuonyesha mfano hali ambayo itawahamasisha na wanawake wengine kufanya vizuri katika masomo yao.
“Hata sasa uongozi wa awamu ya Tano tunaye Makamu wa Rais mwanamke Mhe; Samia Suluhu Hassan ambaye anafanya kazi nzuri sana na katika mkoa wetu wa Kilimanjaro tunaye Dkt. Anna Mghwira ambaye ni mama mahiri mwenye kujiamini,” anafafanua Bi. Kinabo.
Pia aliwataka wanawake waongeze ushirikiano na wafanyakazi wanaofanya nao kazi badala ya kutaka kuonekana mabosi muda wote huku akitolea mfano wakati wake akiwa mkurugenzi wa halmashauri mbalimbali hapa nchini.
“Mimi nimefanya kazi kwa miaka 22 nikiwa Mkurugenzi mtendaji katika halmashauri mbalimbali hapa nchini, nilipokuwa kiongozi sikuamini katika kukwamishwa katika nafasi yangu, kwenye sehemu yangu ya kazi nilikuwa na nyenzo, watu, fedha, vifaa niliweza kuvitumia vizuri na nikiwa na tatizo nilikuwa ninakaa na watumishi wenzangu. Ushirikishwaji katika kazi ni jambo la muhimu sana,” anasema.
Bernadetha Kinabo, mkurugenzi wa zamani wa Manispaa ya Moshi. |
0 Comments:
Post a Comment