Tuesday, May 12, 2020

Nofia yalia tozo zisizo na tija

Shirikisho la Viwanda vya Mazao ya Misitu Kanda ya Kaskazini (NOFIA) limeonyesha wasiwasi wake kwa serikali kutaka kunyang’anya vibali vya wanachama wake kutokana na sintofahamu inayoendelea inayotokana na tozo zisizo na tija kwenye mazao hayo ya misitu ikiwamo Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).
Akizungumza ofisini kwake mjini Moshi, Katibu wa Nofia Steven Shirima alisema kumekuwa na changamoto 25 ambazo zimekuwa zikiwakabili baina yao na serikali lakini iliyokubwa kuliko zote ni hofu ya kunyang’anywa vibali ambayo inatokana na tozo zisizo na tija hali ambayo inaweza kudidimiza soko la mazao hayo ya misitu.
“Hebu fikiria katika zao moja la misitu kuna kodi mbalimbali ambazo hazina tija, huo mrahaba wa serikali unatuumiza sana wanachama wa Nofia, kuna ushuru wa halmashauri husika, kuna ushuru wa mfuko wa kuendeleza mazao ya misitu, kuna ushuru wa getini lakini mbaya zaidi ni VAT (Kodi ya Ongezeko la Thamani),” alisema Shirima.
Shirima alisema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inapowafuata na kutaka VAT inakiuka maana halisi ya kodi ya ongezeko la thamani kutokana na kwamba mazao hayo ya misitu hayachakatwa, bado yapo kama mali ghafi.
“TRA wamekuwa wakitubana kupitia kodi hii (VAT), jambo ambalo linatishia viwanda hivi vya mazao ya misitu kwa mfano ukitozwa kodi katika mbao bado ikiwa shambani inatufanya tushindwe kuiuza mbao hiyo kwa bei itakayotulipa sisi,” alisema Shirima.
Aidha katibu huyo anayesimamia mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara alisema hofu yao inakuja kutokana na kutokuwepo na mawasiliano mazuri baina yao na serikali kwani kuna wakati serikali imekuwa ikifanya mambo yake bila kuwashirikisha.
“Serikali inatoa vibali kwa wanachama wetu vya misitu hiyo ya serikali, sasa vibali vinakuwa hatarini kufutwa endapo mwanachama hataweza kufanya kwa muda fulani, unaona sasa namna hali inavyokuwa ngumu hivyo tunafanya hivyo hivyo tu mradi tu tusifutiwe vibali huku tukijua haitupi faida,” aliongeza.
Shirima alisisitiza ndio maana hashangazwi na ujio wa samani za chuma katika kila kona za miji, na kwamba wameshakaa na wizara husika kujadiliana juu ya changamoto hizo ili kila upande ufaidike bila kugandamiza upande mwingine kwa maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Hata hivyo alisisitiza mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona yamewayumbisha kwa kiasi kikubwa na kwamba itawachukua muda kurudi katika mstari baada ya janga hilo kudhibitia ipasavyo.

0 Comments:

Post a Comment