Kinyala Johannes Lauwo (1871-1996) |
Kilimanjaro ni jina la mlima mrefu kuliko yote barani Afrika. Mlima huo
upo nchini Tanzania katika Mkoa wa Kilimanjaro. Una urefu wa mita 5,895 (futi
19,340). Ina safu ndogo ya milima mitatu: Kibo, Mawenzi na Shira. Hiyo mitatu
inaonekana kama vilele vitatu vya mlima mmoja, hivyo si vibaya kusema
Kilimanjaro ni mlima.
Kijiolojia Kilimanjaro ni volkeno iliyolala kwa sasa. Kwenye kilele cha
Kibo ambacho kwa sasa kinaitwa Uhuru gesi bado inatoka. Kumbukumbu ya mwisho ya
wenyeji kushuhudia mlipuko ilikuwa mwaka 1730.
Kutokana na maendeleo ya viwanda barani Ulaya katika karne ya 15 ndipo
wazungu wengi kutoka huko walianza kuzuru maeneo mbalimbali kwa kutafuta mali
ghafi kwa ajili ya viwanda vyao. Miongoni mwa maeneo waliyofika ni bara la
Afrika.
Bara la Afrika halikuwa tupu lilikuwa na watu wake waliokuwa na
ustaraabu. Ujerumani ni miongoni mwa mataifa yaliyopambana kutafuta maeneo hata
kufanyika kwa mkutano wa Berlin mwaka 1884 kwa ajili ya kugawana maeneo
miongoni mwa mataifa makubwa ili kusitokee mgongano wa kimaslahi.
Wasomi na wapelelezi waliingia katika maeneo mengi Afrika kwa ajili ya
kufanya utafiti wao miongoni mwao alikuwa Hans Heinrich Josef Meyer ambaye
alikuwa msomi na mwanajiografia wa Ujerumani kutoka mjini Hildburghausen.
Aliingia kwenye vitabu vya kumbukumbu za kihistoria kama raia wa kwanza
kutoka barani Ulaya kufika katika kilele cha mlima Kilimanjaro (Kibo) mnamo
mwaka 1889. Safari ya kupanda iliongozwa na Kinyala Johannes Lauwo baada ya
kupata Baraka za Mangi Marealle I.
Kwa mujibu wa maelezo kutoka katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri la
Ashira, inaelezwa kuwa Kinyala Johannes Lauwo ambaye ni mtoto wa Rawuya Lauwo
alizaliwa mwaka 1871 huko Rengoni Marangu. Kinyala Johannes Lauwo
hujulikana pia kwa jina la Yohani/Yohana Kinyala Lauwo ambaye anachukuliwa kuwa
ni mtu wa kwanza kufika katika kilele cha mlima Kilimanjaro na mtu wa kwanza
kumwongoza mzungu wa kwanza kufika katika kilele cha Uhuru.
Takwimu za kuzaliwa kwake ziliwekwa wazi na binamu wake wa kwanza
Mchungaji Yakobo Paulo Lauwo Juni 1, 1995.
Lauwo alibatizwa Septemba 1, 1918 na Andrew Schone. Mnamo mwaka 1989
serikali ya Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani kwa wakati huo ikiwa ni
Ujerumani Magharibi ilitoa fedha kwa serikali ya Tanzania kwa ajili ya kujenga
nyumba ya Kinyala Lauwo ikiwa ni sehemu ya kukumbuka mchango wake wa kumwongoza
Mzungu wa kwanza kutoka barani Ulaya kufika katika kilele cha mlima Kilimanjaro
mnamo mwaka 1889 Meyer (1858-1929) na Ludwig Purtscheller (1849-1900) kutoka
Austria.
Huyu Ludwig alitajwa siku ya msiba wake kama mpanda mlima mkubwa wa
dunia ambaye alifika katika Kilele cha Uhuru mnamo Okotoba 6, 1889. Kufika kwa
Meyer katika kilele cha mlima Kilimanjaro lilikuwa ni jaribio lake la tatu.
Awali alishindwa baada ya Meyer kumuomba Mangi Marealle I ambaye
alikuwa akitawala katika eneo la Marangu lote kama anaweza kumpata mtu yeyote
mwenye uzoefu na kupanda mlima huo. Mangi Marealle I baada ya maongezi ya muda
mrefu alimteua Kinyala Lauwo ambaye alikuwa kijana mdogo wa skauti ambaye siku
anateuliwa kumwongoza Meyer alikuwa amefikishwa katika mahakama ya Mangi kwa
ajili ya kujibu shtaka dogo lililokuwa likimkabili.
Kwa mujibu wa Meyer mwenyewe katika maandishi yake anasema siku hiyo
alipewa vijana wengine wawili, mapota tisa, mpishi mmoja na mwongozaji alikuwa
Lauwo. Meyer na Purtscheller walifika katika maanguko ya barafu oktoba 3, 1889
na kurudi katika kambi ili kupisha theluji hiyo ipungue makali. Oktoba 6, 1889
walifanikiwa kupita katika eneo hilo lililokuwa na theluji kali na kutinga
katika kilele cha mlima Kilimanjaro. Wakati wanarudi wakagundua kwamba barafu
ile imeshayeyuka hivyo walirudi taratibu bila madhara yoyote.
Kwa maelezo ya mwandishi wa jarida, katibu muhtasi na Mwenyekiti wa
Kilimanjaro Branch of the Historical Association of Tanzania Bernard
Leeman alisema mwaka 1973 alifanikiwa kumwoa mtoto wannne wa Mchungaji Yakobo
Lauwo.
Mke wa Mchungaji Lauwo na mke mkubwa wa Kinyala Lauwo wote wawili
walikuwa na asili ya Kimaasai licha ya kuwa walikuwa katika ukoo wa Kichaga wa
Lyamuya.
Leeman anasema alifanya mahojiano na Kinyala mnamo mwaka 1993 ambapo
mwafrika huyo mwenye rekodi ya kipekee alikuwa akiongea zaidi Kichaga na baadhi
ya maneno ya Kiswahili.
Kwa kinywa chake Kinyala Lauwo alisema yeye alikuwa ni skauti wa jeshi
la Mangi Marealle I ambapo alikuwa akikaa kati ya vilele viwili vya Kibo na
Mawenzi kwa ajili ya kuangalia wavamizi wa mifugo au wapi wanapoweza kupata
kuvamia mifugo katika baadhi ya jamii zilizokuwa zikiuzunguka mlima
Kilimanjaro. Wakati akifanya kazi hiyo alikuwa na mabinamu zake wawili
waliombatana naye mara kwa mara.
Kinyala Lauwo aliweka bayana kwamba alijaribu mara tisa kupanda kilele
cha Kibo na kufanikiwa. Katika hizo mara tatu alipanda peke yake hadi kwenye
Crate lakini hakujua kama kulikuwa na eneo jingine kubwa zaidi ambalo volcano
ilikuwa inatoka kwa lugha za kijiografia hufahamika kama Caldera.
Kinyala Lauwo aliwahi kuwambia Leeman kuwa alishawahi kumuona Chui
aliyekufa lakini hakujua kuhusu hadithi ya maarufu za Hemingway. Sasa baada ya
Meyer na Purtscheller kurudi katika kambi Kinyala Lauwo ndipo alipojua kuwa
kuna shimo katika kipande cha barafu (glacier) kwa sasa mahali hapo
panafahamika kwa jina la Johannes Notch. Hapo pana uwazi mkubwa kati ya mapande
ya barafu ya Ratzel na Rebamman.
Kinyala Lauwo alikuwa na wake wawili. Pia aliwahi kufanya kazi ya
kuongoza wapanda mlima na Hotel ya Kibo hadi miaka ya mwanzoni ya 1990.
Alifanikiwa kuzaa watoto watatu wa kike. Leeman aliandika katika rekodi zake
kuwa Kinyala Lauwo alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 125 na kwanza rekodi
ya umri wake aliipeleka katika vitabu maarufu vya rekodi ulimwenguni vya
Guinness Book of Records. Jarida la Canberra Times la Australia lilishawahi
kuandika habari kuhusu Kinyala Lauwo na umri wake.
Kinyala Lauwo alizaliwa mwaka 1871 na kufariki dunia Mei 10, 1996. Kwa
asili neno Lauwo lina maana ya “Tazama Mapambazuko”. Lauwo ni ukoo ulioanzia
ardhi ya Ukamba ambapo mwanzilishi wake alimwoa Matesha ambaye alifanikiwa
kuzaa watoto wa kike na wa kiume. Watoto wote wa kiume huitwa Lauwo na wa kike
huitwa Matesha. Baada ya hapo akafuata Kimonge kutoka Umaasai, ambaye alimzaa
Aisere (kaka yake alifahamika kwa jina la Kimemia) aliyekuja kumzaa Mramba
kisha Mwiwere. Mwiwere akamzaa Rawi aliyekuwa na kaka aliyefahamika kwa jina la
Mkawo. Rawia akamzaa Kinyala mwaka 1871. Kimemia aliwazaa Kiwere na Ndauliso
wakati Rawia aliendeleza ukoo wake ambao ulikuja kuwazaa Mkawo, Paolo na Yakobo
(1915-2000).
0 Comments:
Post a Comment