Taarifa kuhusu kifo cha Adolf Hitler zilikuwa zikitunzwa kama siri kwa
miaka mingi hadi mwisho wa Ukomunisti (Urusi) na ndio sababu kulikuwa na uvumi
wa kwamba Hitler hakufa na labda alikimbilia hadi Amerika Kusini. Hiyo ilitokana
na idadi kubwa ya wasaidizi wake waliofaulu kutoroka.
Gazeti la nchini Marekani
"Stars and Stripes" la Mei 2, 1945 lilitangaza kifo cha mbabe wa
Ujerumani Adolf Hitler.
Kwa uchache ni kwamba baadhi ya maafisa wa jeshi ya
Ujerumani walipanga mara kadhaa kumwua Hitler. Julai 20, 1944 Kanali Stauffenberg
alilipusha bomu katika Ikulu ya Hitler pale Prussia ya Mashariki.
Hitler
alijeruhiwa lakini hakufa. Kitendo hicho kilimfanya Hitler ahame. Hivyo kuanzia
Januari 1945 Hitler alihamia tena Berlin kutokana na uvamizi wa jeshi la Kirusi
katika Ujerumani Mashariki.
Hapa alikaa katika boma imara chini ya ardhi.
Hakutoka mjini humo tena. Mnamo Aprili 20, 1945 Hitler alishehereka mara ya
mwisho kumbukizi kuzaliwa na kupokea wageni wachache.
Siku iliyofuata vikosi
vya kwanza vya jeshi la Urusi vilianza kuingia katika maeneo ya Jiji la Berlin.
Aprili 25, 1945 Berlin yote ilizungukwa kama kisiwa na jeshi la Wasovieti na
tangu Aprili 28, 1945 waliingia katika kitovu cha Berlin.
Hitler bado alikuwa
na tumaini kwamba vikosi vya jeshi la Kijerumani kutoka magharibi vitafika
Berlin lakini majaribio yote yalishindikana. Habari zilipokelewa Berlin ya
kwamba makamu zake Hitler Himmler na Goering walijaribu kutafuta mapatano na
Marekani au Uingereza.
Hitler aliwatangaza ni wasaliti akaamuru kuwakamata
lakini amri hizi hazikutekelezwa tena maana hawakuwa karibu naye. Katika hali
hii Hitler alielewa ya kwamba hakuna njia ya kushinda na wataalamu na
wanahistoria hukubaliana ya kwamba hapo aliamua kujiua.
Usiku wa Aprili 27,
1945 alimwoa mpenzi wake wa miaka mingi Eva Braun. Aliendelea kutunga wosia
wake ambamo alimtaja mkuu wa jeshi la maji Karl Doenitz kuchukua madaraka yake
kama mkuu wa dola na wa jeshi.
Mnamo Aprili 29, 1945 jioni alipokea habari ya
kwamba Fashisti Benito Mussolini wa Italia ameuawa nchini mwake.
Aprili 30,
1945 aligawa sumu kwa wote waliokuwa pamoja naye katika boma chini ya ardhi
akawaruhusu kuondoka; aliagiza sumu ijaribishwe kwa mbwa wake mpendwa
"Blondi".
Mnamo saa 15.30 Eva Brau alijiua kwa kumeza sumu na Hitler
alijipiga risasi kichwani. Wasaidizi wa mwisho walibeba maiti hadi bustani ya
ikulu na kuziweka katika shimo kutokana na mlipuko wa bomu; hapa wakazichoma
kwa petroli.
Warusi waliingia saa chache baada ya vifo hivi. Walikuta maiti ambapo
Mei 5, 1945 bila kutambua ni Hitler na Eva Braun. Mnamo Mei 10, 1945 msaidizi
wa daktari wa meno wa Hitler aliweza kutambua maiti kutokana na meno.
Mabaki
yalizikwa baadaye karibu na makao makuu ya jeshi la Kirusi katika Ujerumani ya
Mashariki; yalihamishwa mara kadhaa kila wakati makao makuu yalipohamishwa.
Mwishoni mabaki ya maiti yalichomwa na Warusi Aprili 5, 1970, majivu yalisagwa
na yote kutupwa katika mto mdogo karibu na mji wa Magdeburg.
0 Comments:
Post a Comment