Kampuni ya Utalii mkoani Kilimanjaro Blue Art Studio imetoa msaada wa chakula kwa wafanyakazi wake katika kipindi hiki wakati dunia na mataifa mbalimbali yakiendelea na utafiti wa chanjo dhidi ya Covid-19.
Akizungumza na gazeti hili Mkurugenzi wa Blue Art Studio Reagan Balozi alisema kilichomfanya awapatie chakula cha kujikimu wafanyakazi wake ni kutokana na hali ya sasa ya biashara ya utalii ambayo imefungwa kutokana janga la corona ambapo wafanyakazi wote wa sekta hiyo wapo majumbani.
Balozi alisema kilichomsukuma kuwapa wafanyakazi wake chakula ni suala la utu na haki za mfanyakazi ambapo baadhi ya makampuni yamepunguza wafanyakazi kutokana na janga la corona hali ambayo inawaweka mahali pagumu wafanyakazi hao.
“Sipendi kuona mfanyakazi akipata taabu wala familia yake ikihangaika, wafanyakazi wangu niliwafanya kama familia tulikuwa pamoja wakati wa furaha, wakati wa shida sio vizuri kukimbia na kujiokoa mwenyewe,” alisema Balozi.
Mkurugenzi huyo alisema wakati janga hilo la corona lilipoanza aliandaa programu ya mafunzo kwa wafanyakazi wake namna ya kujikinga na maradhi hayo hasa ikizingatiwa utalii wao umekuwa ukilenga zaidi watu kutoka nje na kwamba wao wangekuwa wa kwanza kuathirika na maradhi hayo.
“Niliandaa vipindi vinne vya elimu kuhusu corona wakati ilipokuwa ikianza huko China, utalii wetu umekuwa ukilenga zaidi watu wa nje nilianza kufundisha wafanyakazi wangu namna gani ya kujilinda kimwili, kiuchumi na familia zetu,” alisema Balozi.
Balozi alisema haijulikani lini corona itamalizika na hatima yake kwa uchumi wa mmoja mmoja, makampuni, nchi na dunia kwa ujumla huku akisisitiza ulazima wa kujiongeza kwani utalii mpaka utakapokuja kusimama kuna uwezekano ukachukua muda mrefu.
“Binafsi nimewapa wafanyakazi wangu chakula cha kuwatosha mwaka mzima, sijawafukuza. Chakula hicho nilikilima mwaka mmoja uliopita na nilishindwa kuuza nikaamua kuhifadhi sasa nilipoona kuna shutting down ya kampuni kutokana na corona nikafikiria namna wafanyakazi wangu watakavyoweza kuishi na ndivyo ambavyo nimefanya,” alisema Balozi.
Hata hivyo Balozi aliongeza kuwa hata kama corona itamalizika ameandaa mpango mwingine wa kuwanusuru wafanyakazi wake kwa kuwapeleka katika kilimo biashara kutokana na kwamba asilimia 70 ya wafanyakazi wake wana uzoefu wa kilimo na asilimia 30 wengi wao ni watu wa mauzo ambapo atawatumia katika mauzo ya bidhaa zinatokanazo na kilimo.
“Kiuchumi tupo kwenye wakati mgumu, bado tupo katikati ya vita; hata kama corona itamalizika utalii hautaweza kusimama mara moja, wafanyakazi wangu nitawapeleka kwenye kilimo biashara,” aliongeza Balozi.
0 Comments:
Post a Comment