Sunday, May 3, 2020

TEF yataka uwazi taarifa ya Covid-19


Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limetaka utashi wa kisiasa katika kuamua hatma ya uhuru wa vyombo vya habari na wanahabari wakati huu ambao dunia inapambana na maradhi ya corona huku utoaji wa taarifa kuhusu hali ya maradhi hayo ikiendelea kuminywa.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Idhaa ya Kiswahili ya DW kuelekea siku ya Vyombo vya Habari ambayo hufanyika kila mwaka Mei 3, Katibu wa Jukwaa la Wahariri Neville Meena alisema kumekuwa na hofu kubwa kwa vyombo vya habari na wanahabari wenyewe katika utoaji wa taarifa kutokana na hali ya kisiasa nchini iliyopo kwa sasa.

“Hakuna mwandishi wa habari ambaye kwa sasa anaweza kufanya kazi bila hofu, kila mmoja anajaribu kujiponya kwa namna yake,” alisema Meena

Meena alisema wanahabari na vyombo vyao wamekuwa na hofu akifananisha uoga na hofu hiyo kama msemo wa Kiswahili wa kunguru mwoga huponya bawa lake.

“Hali iliyopo kwa sasa kila mmoja anataka kujiponya mwenyewe kwa namna yake kama msemo wa kunguru mwoga huponya bawa lake,” alisema Meena.

Pia Meena aliwaataka wanasiasa kutambua kuwa utashi wao wa kisiasa ndiyo hatma ya nchi nzima katika maendeleo yake ikiwamo uhuru wa wanahabari kuandika taarifa zao bila upendeleo wakiziangatia maadili ya uandishi wa habari.

Meena alisema kinachoonekana sasa ni taarifa nyepesi kutokana kila mmoja katika chombo chake cha habari kuingiwa na hofu ya maisha yake.

Meena hakusita kugusia kupotea kwa mwandishi wa habari wa gazeti la Mwananchi Azory Gwanda ambaye mpaka sasa hakuna taarifa za aliko tangu Novemba 21, 2017.

“Mpaka leo hakuna taarifa kutoka vyombo vya ulinzi na usalama kutuleza aliko Azory Gwanda, huenda ndio sababu waandishi wa habari wanahofu,” alisema Meena.

Katibu huyo aliongeza kuwa bado mashinikizo kila upande yanaendelea kufanyika kwa serikali ili itoke taarifa za kupotea kwa mwandishi huyo huku wengi wakishindwa kuelewa kama Gwanda anaweza kuwa hai au la.

Katika suala la sheria za nchi kuhusu vyombo vya habari Meena alisema Sheria ya Huduma ya Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 bado ni kikwazo kikubwa cha kumfanya mwandishi atekeleze majukumu yake ya kuuhabarisha umma kwa kutoa taarifa sahihi zilizochakatwa kwa umakini wote bila kuficha jambo.

Kauli mbiu ya mwaka huu inasema, “Uandishi wa habari bila Hofu au Upendeleo.”

Siku ya Vyombo vya Habari dunian ilitangazwa katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa Desemba 1993 kutokana na Mkutano mkuu wa UNESCO uliofanywa na kuibua Azimio la Windhoek Oktoba 1992.

Maadhimisho ya mwaka huu yanafanyika huku kukiwa na kitisho cha corona ambacho kimekwaza dunia kwa ujumla katika sekta zote.


0 Comments:

Post a Comment