Umoja wa Wanawake
Tanzania , Jumuiya ya Chama Cha Mapinduzi (UWT) wa Manispaa ya Moshi wametoa
misaada mbalimbali ya kibinadamu ikiwemo vyakula na sabuni kwa waathirika wa
mafuriko katika kata ya Mji Mpya iliyopo Manispaa hiyo.
Akizungumza
wakati wa kukabidhi misaada hiyo kwa kaya 323 zilioathirika na mafuriko katika
kata hiyo, Katibu wa UWT Manispaa ya Moshi, Bi. Shakila Bakari Singano
alifafanua kuwa, UWT imejitolea kutoa misaada hiyo ya kibinaamu kwa kutambua
adha wanazokumbanazo waathirika hao, hasa akinamama, wazee na watoto.
“Katika mafuriko
hayo walioathirika zaidi ni akinamama, wazee na watoto, hivyo basi
wenzetu walipotueleza kuhusiana na janga hili kamati ya utekelezaji ya
UWT Manispaa ya Moshi mjini, tukaona ni muhimu kuwajali wenzetu waliopatwa na
mafuriko kwa kuwapatia misaada mbalimbali ya kibinadamu ikiwemo chakula na
sabuni za kufulia,” alifafanua Singano.
Kwa upande wake
Kaimu Mwenyekiti ya UWT Moshi Manispaa Witines Mziray, aliitaja baadhi ya
misaada waliyoitoa kwa kata ya Mji Mpya, kuwa ni pamoja na magunia 15 ya
mahindi, maharagwe kilo 150, na sabuni katoni 9, vyote vikiwa na thamani ya
shilingi milioni 1.8/-.
Aliendela
kufafanua kuwa, mitaa mitatu ya kata hiyo ndiyo iliyoathiriwa zaidi na mafuriko
hayo ambapo kila mtaa umepata gunia tano za mahindi na maharagwe kilo 50 na
katoni tatu za sabuni.
“UWT imeguswa na kuona ni vyema kuwakimbilia katika kipindi hiki cha matatizo ya mafuriko,” alifafanua Mziray.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi, Michael Mwandezi, Mchumi wa Manispaa hiyo, Monica Sana alitoa shukrani za dhati kwa UWT kwa moyo wa huruma waliouonyesha kwa kuwajali wananchi wa kata ya Mji Mpya kwa tatizo la mafuriko lililowakumba hivi karibuni.
“Kwa niaba ya
serikali Manispaa ya Moshi tunatoa shukrani kwa UWT kwa kutuunga mkono
kuwasaidia wahanga wa mafuriko, napenda kusema kwamba chakula hiki pamoja na
sabuni vitagawanywa kwa utaratibu mzuri na kwa walengwa,” alifafanua Mama Sana.
Aliongeza kuwa,
misaada hiyo itafika mahali husika na kumtaka Afisa Mtendaji (WEO) kata hiyo
Kago Nyanda, kutoa taarifa ya mgawanyo wa misada hiyo ya kibinadamu kwa kata
yake pamoja na kutoa nakala kwa mwenyekiti wa UWT Moshi Maniapaa.
Kwa upande wake
Afisa Mtendaji wa kata hiyo, Kago Nyanda aliwashukuru UWT kwa msaada huo wa
kibinadamu na kufafanua kuwa utafika kwa walengwa kama ilivyokusudiwa.
Aliendelea
kufafanua kuwa, jumla ya kaya 323 zimeathirika sana na mafuriko hayo
yaliyotokea Aprili 21 mwaka huu ambapo nyumba 18 zilibomoka kabisa, huku athari
nyingine kubwa zilizojitokeza katika mafuriko hayo ni baadhi ya wananchi kukosa
makazi huku wengine wakikosa chakula kutokana na chakula walichokuwa nacho
kusombwa na mafuriko hayo.
0 Comments:
Post a Comment