Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga imeanzisha mpango mkakati wa
kudumu wa kuiwezesha misitu na mabwawa yaliyopo wilayani humo kuwa raslimali
zitakazofungua fursa za maendeleo kwa wananchi wake na kuongeza kipato kwa
halmashauri hiyo tofauti na ilivyo sasa.
Akizungumza ofisini kwake hivi karibuni Mkuu wa Wilaya ya Mwanga
Thomas Apson alisema mabwawa yatakayohusika na mpango huo ni Nyumba ya Mungu,
Jipe, Kisanjuni pia Misitu ya Kambi ya Nyuki, Toloha na Kirya.
“Tumekaa tupo katika hatua za awali, tumeamua wataalamu waingie
kazini kufanya tathmini ya mahitaji ya jamii wananchi nao wakiridhia wanaweza
kutoa ushirikiano kwa maana msipokubaliana unaweza kuzua mgogoro na kwenda
kushtakiana kwa mabosi wetu kwa mheshimiwa Waziri Mkuu au Rais, jambo ambalo
halitakuwa zuri,” alisema Apson
Mkuu wa wilaya huyo alisema, mpango huo utawashirikisha wataalam wa sekta za nyuki, samaki na wananchi katika utekelezaji wake ikiwemo ujenzi wa nyumba za kuhifadhia mizinga ya nyuki ili kurahisisha ufugaji wa nyuki na kuongeza uvunaji wa asali kwa wingi.
Apson aliweka bayana faida zitakazopatikana baada ya mpango huo
utakapoanza kufanya kazi ikiwamo ajira kwa vijana zitakazotokana na uvuvi na
uchuuzi wa samaki kutoka katika mabwawa pia mapato katika halmashauri hiyo
yataongezeka hali ambayo itainua uchumi wa wilaya.
“Tunakwenda kuiboresha Halmashauri yetu ya Mwanga kupitia vyanzo
vyake yenyewe kupitia ushuru ambao utakuwa unapatikana, tutaacha utegemezi wa
Bwawa la Nyumba ya Mungu pekee katika kujipatia mapato ya ndani ya Halmashauri
yetu,” alisema Apson
Kwa upande wake Mhadhiri wa Chuo kikuu cha Dodoma Dkt. Ombeni
Msuya alisema bwawa la Kisanjuni litaandaliwa mpango wa kuwawezesha wananchi
kufuga samaki katika vizimba baada ya kuonekana matumizi ya awali kutoleta tija
ipasavyo.
Mkuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi wa Wilaya hiyo Emmanuel Sindijo alisema, serikali za vitongoji, vijiji, kata na wananchi zitashirikishwa katika hatua zote bila kuathiri shughuli zao za kila siku.
0 Comments:
Post a Comment